Na Hassan Kingu
Tuwalaumu makipa, Ali Ahmada wa Azam na Razack Sekimweri wa Mtibwa kwa kufungwa mabao katika mechi zao na Yanga lakini tusisahahu kumpongeza Stephane Aziz Ki, ameendelea kudhihirisha uwezo wake wa kufunga au kutengeneza mabao ya mashuti ya mbali.
Makipa hawa wawili wote wamekutana na uwezo wa Aziz Ki na wakajikuta wakiziumiza timu zao na kutupiwa zigo la lawama kwa kuruhusu timu zao zipoteze pointi katika mechi ambazo kulikuwa na kila dalili za kugawana pointi.
Kama si shuti la Aziz Ki, Azam na Yanga pengine zingemaliza mechi kwa matokeo ya mabao 2-2, ni hivyo hivyo katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar nayo huenda ingeisha kwa sare tasa ya 0-0 lakini ni Aziz Ki aliyesababisha bao pekee la Yanga.
Si Sekimweri na Ahmada peke yao waliokutana na zahma kutoka kwa Aziz Ki, orodha hiyo ina kipa mwingine mahiri nchini, Tanzania One, Aishi Manula naye yumo, tena huyu aliumizwa kwenye Dar Derby ambayo pengine ingeisha kwa Simba kutoka na ushindi wa bao 1-0.
Hii maana yake ni kwamba uwezo ambao Aziz Ki ameudhihirisha haujaishia katika mechi ambazo unaweza kuzitaja kuwa ni za kawaida, zisizo na ushindani na ambazo Yanga inakuwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi, bali mechi kubwa na ambayo matokeo yake yanateka hisia za mashabiki walio wengi ndani na hata nje ya nchi. Naizungumzia Dar Derby.
Nini kiliwaponza
Kwa mtazamo wangu makipa hawa wote waliponzwa na mahesabu, makadirio yao hayakuwa mazuri wakati Aziz Ki akipiga mpira au waliponzwa na ‘poor timing’. Wote mashuti ya Aziz Ki yaliwababatiza au kuwagonga, Sekimweri mpira ulimbabatiza na kujaa wavuni wakati Ahmad mpira ulimgonga na kumkuta mfungaji mwingine aliyeujaza wavuni.
Wakati Sekimweri mpira ukimgonga miguuni, Ahmada yeye ulimgonga kifuani/begani na wote wamejikuta wakilaumiwa, si kwa poor timing bali wapo mashabiki wanaohisi kwamba ni mabao ya mchongo, kwamba walizembea makusudi ili wafungwe.
Hisia
Wanaojenga hoja hiyo wengi wao kama si wote hawana ushahidi wowote bali wanaongozwa na hisia, hawaamini kama kipa anaweza kufungwa bao ‘kirahisi’ namna ile lakini wanasahau kwamba mpigaji tayari amedhihirisha kuwa na uwezo wa kufunga mabao au kupika mabao katika mazingira yale, hawaizungumzii kasi ya mpira ilikuwaje.
Wako wanaojiaminisha kwamba makipa wale wangeweza kuudaka kiulaini mpira uliopigwa na Aziz Ki lakini sina hakika kama wanaijua kasi ya mpira au nguvu alizotumia mpigaji wakati anaupiga mpira ule, nimeona mara kadhaa makipa mahiri mipira ya aina ile wanaiokoa kwa kutumia ngumi kwa kuurudisha uwanjani au kutoa kona, si kuudaka.
Hadithi ya mabao ya mchongo bado inanipa shida kuiamini hasa kwa kuwa wanaosimamia hoja hiyo imani yao imejengwa na hisia zao na katika hali ya kawaida kila mtu ana haki ya kujenga hisia lakini hawana ushawishi wa aina yoyote kumfanya mtu akubaliane nao katika jambo hilo na zaidi ya hilo wengi kama si wote wanaukubali ukweli kuhusu ubora wa Aziz Ki.
Wakati mwingine pia ni muhimu tunapojenga hisia hasa zilizo mbaya tufikirie mara mbili na tujiulize kuhusu mabeki wa makipa hawa kwa kuwa mpira wa adhabu au penalti inapopigwa ndani ya dakika 90 mabeki wanatakiwa kuwa tayari kwa lolote hasa mpira unapogonga mwamba au kuokolewa na kipa na kurudi ndani kama ilivyokuwa kwa Ahmada.
Mpira uliopigwa na Aziz Ki na kurudi uwanjani ulimkuta mchezaji wa Yanga ambaye hakupata misukosuko ya mabeki wa Azam, alifunga, vipi hapa hatuoni kama na mabeki nao hawakujipanga vizuri hasa kwa kutambua uwezo wa mpigaji mpira?
Ukiachana na Ahmada na Sekimweri, Manula naye ni hivyo hivyo aliponzwa na poor timing kwani picha zimemuonesha namna alivyokuwa akiwapanga mabeki wake hadi kujiridhisha mwenyewe na kutoa ishara ya dole gumba akimaanisha hapo sawa lakini nini kilimkuta? Alitunguliwa na Aziz Ki.
Yote kwa yote tuendelee kuwalaumu makipa hawa lakini tunapoamua kujenga hisia mbaya dhidi yao tuwe na ushahidi au hoja zinazojitosheleza, tofauti na hivyo tuna wajibu wa kumpongeza mpigaji, kumpongeza Aziz Ki kwani ameendelea kudhihirisha kwamba ana uwezo wa kufunga au kutengeneza mabao kwa mashuti ya mbali.
Soka Tumpongeze Aziz Ki tukiwalaumu makipa
Tumpongeze Aziz Ki tukiwalaumu makipa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
