Na mwandishi wetu
Klabu ya Singida Big Stars au Singida Fountain Gate, imempa mkataba wa miaka miwili beki wa kati wa timu hiyo, Joash Onyango utakaoanza kutumika baada ya kumalizika mkataba wa mkopo kutoka Simba alionao sasa.
Onyango raia wa Kenya alijiunga na Singida mwanzoni mwa msimu huu kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Simba SC.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo iliiambia GreenSports leo Ijumaa kuwa tayari imemalizana na mchezaji huyo ambaye kama angemaliza mkopo wake angebaki kuwa mchezaji huru sababu pia angekuwa amemalizana na Simba.
“Tayari tumemalizana na Onyango kwamba hata muda wa mkopo ukimalizika, ataendelea kubaki hapa kutokana na mkataba mpya wa miaka miwili tuliompa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza alisema taarifa hizo hazijamfikia kwenye idara yake, akifafanua kama kutakuwa na lolote kuhusiana na hilo basi wataliweka wazi mapema.
Hata hivyo, Onyango amekuwa nje ya uwanja akikosa mechi tatu mfululizo sasa, akisumbuliwa na majeraha ya misuli ya paja aliyoyapata kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC ya Misri iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wiki tatu zilizopita.
Soka Onyango apewa miaka miwili Singida
Onyango apewa miaka miwili Singida
Read also