Istanbul, Uturuki
Kocha wa Inter Milan, Simone Inzaghi amesema anajivunia mafanikio ya timu yake licha ya kushindwa kutamba mbele ya Man City katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana Jumamosi.
Inter Milan jana ililala kwa bao pekee la Man City lililofungwa na Rodri dakika ya 68 na kuifanya City ambayo pia ni kinara wa Ligi Kuu England (EPL) ibebe kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa.
Inzaghi (pichani juu) hata hivyo hajakata tamaa na matokeo hayo akidai ameiongoza timu katika msimu mgumu uliojaa presha na hatimaye akaiwezesha kushika nafasi ya tatu katika Serie A na kubeba mataji ya Super Cup na Italia Cup.
“Usiku kama huu (Jumamosi) siwezi kuwataja wachezaji japo mmoja ambaye amecheza chini ya kiwango, nilisema jana (Ijumaa) sitoweza kumbadili mchezaji kwa yeyote na leo dunia nzima imeona ni kwa nini nilisema hivyo,” alisema Inzaghi.
“Wameoionyesha duniani yote ni kwa kiasi gani walivyoweza kuizuia Manchester City, kikosi ambacho kila mtu anajua kina wachezaji wa viwango vya juu,” alisema Inzaghi.
“Niliwakumbatia wachezaji wangu mmoja baada ya mwingine, kwani walikuwa wa kipekee ni kama jinsi mashabiki wetu walivyokuwa na walikuwa na haki ya kupata matokeo tofauti lakini ni matumaini yangu kwamba walikuwa na furaha kwa namna timu yetu ilivyocheza,” alisema Inzaghi.
“Mimi na wachezaji wangu tulikumbana na lawama na nikiri kwamba kuna mechi tulizopoteza ambazo hatukutakiwa kupoteza lakini nafikiri tulipata somo zuri katika mechi tulizopoteza,” alisema na kuongeza kuwa timu yake imeshinda mataji manne katika kipindi cha miaka miwili.
“Kwa ari, mshikamano na matumaini tuliyonayo, nafikiri tutakuwa katika hatua hii kwa mara nyingine siku zijazo,” aliongeza Inzaghi.