Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp amesema kwamba mzozo ulioibuka kati yake na mshambuliaji wake, Mohamed Salah mwishoni mwa wiki iliyopita katika mechi yao na West Ham haupo tena.
Klopp na Salah walionekana katika picha za televisheni wakitoleana kauli zilizoashiria kuwapo mzozo baina yao wakati wa mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Baada ya mechi hiyo, Salah ambaye alizozana na kocha wake wakati akiingia uwanjani kutokea benchi, alisema kwamba ‘moto ungeweza kuwaka’ iwapo angeamua kuzungumza kilichojiri.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana Ijumaa, Klopp hakutaka kuelezea kwa nini waliingia katika mzozo yeye na mchezaji wake badala yake alisisitiza kwamba jambo hilo limepita na kwa sasa wanaangalia mbele.
“Yote yamemalizwa, hakuna tatizo, kama tungekuwa hatujuani kwa muda mrefu sina hakika kama tungeweza kulifanyia kazi suala hilo, lakini tunajuana kwa muda mrefu na vile vile tunaheshimiana,” alisema Klopp.
Klopp alisisitiza kwamba hakuna tatizo na mambo ya aina hiyo wanaweza kuyamaliza wao wenyewe bila ya kuwapo matarajio ya kuingiliwa na watu wengine wa nje.
Sare dhidi ya West Ham imezidi kufifisha matumaini ya Liverpool kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) kwani kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa imeachwa na vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi tano zikiwa zimebaki mechi tatu kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.