Rio de Janeiro, Brazil
Makocha, Pep Guardiola na Carlo Ancelotti wameanza kutajwa kwa mmoja wao kumrithi kocha wa Brazil, Tite aliyejiuzulu ingawa nyota wa zamani wa timu hiyo, Rivaldo anapinga kocha asiye raia wa Brazil kupewa timu hiyo.
Tangu Tite atangaze kujiuzulu baada ya Brazil kutolewa na Croatia katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia, habari za mrithi wa kocha huyo zimeanza kuvuma ambapo jana Jumatatu majina ya makocha hao yamekuwa yakijadiliwa.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa ya Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) ilieleza kuwa shirikisho hilo linasubiri hadi Januari 2023 ili kumtangaza mrithi wa Tite.
Kwa upande wake, Ancelotti ambaye kwa sasa anainoa Real Madrid alikana kuwa na taarifa zozote kuhusu mpango huo na kuongeza kuwa kwa sasa anafurahia mkataba alionao na klabu hiyo ya Hispania unaofikia ukomo Juni 2024 na aliwahi kusema kwamba huenda Real Maadrid ikawa kazi yake ya mwisho kabla ya kustaafu.
Taarifa ya CBF pia ilieleza kuwa mbali na kutambua kwamba nafasi ya Tite ipo wazi lakini hawajampa madaraka mtu yeyote ndani au nje ya shirikisho hilo kutafuta kocha wa kuifundisha timu ya Brazil na kwamba taarifa ya mrithi wa Tite itatangazwa Januari 2023.
Baada ya kuwapo ripoti za CBF kusaka kocha asiye raia wa Brazil akiwamo pia Pep na Abel Fereira, Rivaldo amesema kwamba kumpa mgeni kazi hiyo ni kukosa heshima
“Mrithi wa Tite ni lazima awe Mbrazili, mwenye damu ya Brazil inayokimbia kwenye misuli yake, naamini tuna makocha wanaoweza kuiongoza timu ya Taifa ya Brazil katika kipindi hiki na kufanya kazi nzuri,” alisema Rivaldo.
“Kumleta kocha wa kigeni si uhakika kwamba tutakuwa mabingwa wa dunia, ni kweli kwamba kuna makocha wazuri wasio Wabrazili lakini Selecao (timu ya Brazil) ni yetu, ni ya taifa na lazima iongozwe na mtu mwenye damu ya Brazil katika mishipa yake,” alisema nyota huyo aliyetamba zaidi na timu hiyo mwaka 2002 ilipotwaa ubingwa wa dunia.
Nyota mwingine wa Brazil, Ronaldo de Lima alikuwa na maoni tofauti na Rivaldo akisema anaunga mkono kocha wa kigeni, “Kuna majina makubwa ya makocha wanaoweza kufanya vizuri, Ancelotti, Abel wa Palmeiras, Mourinho wa Roma, hayo ni majina makubwa na wote wana mikataba, sijui CBF watafanya nini ila kwa maoni yangu naunga mkono kocha wa kigeni.”
LigiKuu Pep, Ancelotti watajwa Brazil
Pep, Ancelotti watajwa Brazil
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
