Na mwandishi wetu
Simba imeianza michuano ya Ligi ya Soka Afrika (AFL) kwa sare ya mabao 2-2 na Al Ahly ya Misri katika mechi ya uzinduzi wa michuano hiyo iliyopigwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Fifa na CAF, wageni Ahly walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 45 lililofungwa na Slim na kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele.
Kipindi cha pili Simba ilikianza kwa kufanya mabadiliko ikiwatoa Muzamir Yassin na nafasi yake kuingia Sadio Kanoute na kumtoa Luis Miquisson na nafasi yake kuchukuliwa na Jean Baleke.
Mara baada ya kuanza kipindi cha pili Ahly walifanya shambulizi langoni mwa Simba kabla ya Simba kujibu mapigo lakini ilikuwa vigumu kuwapenya Ahly waliojazana nyuma kulinda lango lao huku wakijaribu kufanya mashambulizi machache.
Simba wakicheza kwa umakini walifanikiwa kuipenya safu ya ulinzi ya Ahly na kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 53 lililofungwa na Kibu Dennis.
Bao hilo lilianzia kwa pasi ndefu ya Saido Ntibazonkiza na kuunganishwa na Baleke kabla ya kumkuta Clatous Chota Chama ambaye aliurudisha ndani mpira wa juu ambao ulikuwa ukitoka nje na kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni kwa kichwa na mpira kumshinda kipa El Shanawy wa Ahly.
Dakika saba baada ya Simba kusawazisha bao hilo, Kanoute aliongeza bao la pili kwa kichwa akiujaza wavuni mpira wa kona uliopigwa na Saido Ntibazonkiza na mfungaji kumzidi ujanja beki wa Ahly aliyekuwa karibu naye.
Iliwachukua Ahly dakika mbili kuwanyamazisha mashabiki wa Simba waliokuwa katika hali ya furaha baada ya kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Mahmoud Kehraba.
Simba iliendelea kuonesha uhai licha ya kufungwa bao hilo na katika dakika ya 75, Ntibazonkiza aliinasa pasi ya Chama na kupiga shuti la mbali ambalo mlinda mlango wa Ahly, El Shanawy alionekana kuudharau mpira ambao uligonga mwamba wa juu na kuwainua vitini mashabiki wa Simba.
Kocha wa Simba, Robertinho aliendelea kufanya mabadiliko akiwatoa Kibu Dennis na nafasi yake kuingia Willy Onana na Shomary Kapombe na nafasi yake kuchukuliwa na Israel Mwenda.
Wakati Simba wakipambana kusaka bao la tatu, Ahly walikuwa wakijihami zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kama si umakini wa safu ya ulinzi ya Simb a na kipa Ally Salim timu hiyo ingeweza kupata bao la tatu.
Zikiwa zimebakia dakika chache mpira kumalizika, kocha Robertinho alimtoa Chama na nafasi yake kuingia John Bocco, mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Mechi ya leo ambayo ni ya uzinduzi wa michuano mipya ya AFL ilihudhuriwa na Rais wa Fifa, Gianni Infantino na rais wa Caf, Patrice Motsepe.
Wengine waliokuwa uwanjani ni mkurugenzi wa maendeleo ya soka wa Fifa na kocha wa zamani wa Arsenal, Arsenal Wenger, mwamuzi maarufu wa zamani wa Fifa ambaye pia mwenyekiti wa kamati ya waamuzi ya Fifa, Pierluigi Collina na viongozi mbalimbali wa soka barani Afrika.
Kimataifa Simba, Al Ahly zatoka sare AFL
Simba, Al Ahly zatoka sare AFL
Read also