Manchester, England
Kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo amesaini mkataba mpya ambao utafikia ukomo mwaka 2031 hali ambayo inamaliza utata uliotawala siku za karibuni kuhusu mambo ya baadaye ya mchezaji huyo.
Maino, 21 ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England amekubali ofa hiyo baada ya kuibukia kikosi cha kwanza mwaka 2023 katika mkataba ambao ulitarajiwa kufikia ukomo mwaka 2027.
Mambo yalikuwa magumu kwa Mainoo wakati timu hiyo ikinolewa na kocha Ruben Amorim, hali ambayo ilimfanya alazimishe kuuzwa kwa mkopo katika klabu ya Napoli ya Italia wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari.
Mabosi wa Man United hata hivyo hawakuwa tayari kwa jambo hilo na kuweka wazi kuwa klabu hiyo inajua thamani ya Mainoo na kumtaka abaki na apiganie nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Mara baada ya kuondoka kwa Amorim Januari mwaka huu, Mainoo ameanza kikosi cha kwanza mechi 11 chini ya kocha wa muda Michael Carrick na alikosekana katika mechi dhidi ya Leeds kwa kuwa alikuwa majeruhi, mechi ambayo Man United ililala kwa mabao 2-1.
Baada ya kusaini mkataba huo mpya Mainoo alisema kwamba kwa wakati wote Manchester United pamekuwa ni nyumbani kwake na klabu imekuwa na maana kubwa kwake.
“Klabu hii ni ya kipekee, ina maana kubwa kwangu na kwa familia yangu, nina heshima ya kuishi katika ndoto yangu, nikiendelea kuwa mwenye shauku isiyochoka ya kupata mafanikio kama ilivyokuwa wakati nikianza mazoezi hapa mara ya kwanza,” alisema Mainoo.
Mainoo aliongeza kwamba ana shauku kubwa ya kutekeleza jukumu lake la kuisaidia klabu hiyo iendelee kwa wakati wote kupigania mataji kwa miaka ijayo.
