Na mwandishi wetu
Taifa Stars imesonga mbele katika mbio za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) baada ya kuichapa Somalia mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Stars kwa matokeo hayo, imesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya awali iliyochezwa kwenye uwanja huo huo, mechi ambayo Somalia walikuwa wenyeji kutokana na hali ya kiusalama nchini kwao kutokuwa nzuri.
Bao la kwanza la Stars lilipatikana katika dakika ya 33 ya mchezo huo, mfungaji akiwa ni nyota wa Azam, Abdul Sopu aliyejiunga na timu hiyo akitokea Coastal Union, ambaye pia ndiye aliyeifungia Stars bao pekee katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo.
Somalia hawakuonekana kutetereka baada ya kufungwa bao hilo na dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili walipata bao mfungaji akiwa ni Farhan Ahmed lakini dakika 16 baadaye Stars walifuta ndoto za Somalia kutoka na ushindi baada ya kupata bao la pili lililofungwa na Dickson Job.
Kwa ushindi huo Stars sasa imeingia raundi ya pili ambapo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Uganda Cranes kwa kuanzia nyumbani Agosti 26 au 28 kabla ya kumalizia ugenini kati ya Septemba 2 hadi 4.
Stars: Abdultwalib Msheri, Kibwana Shomari, Mohammed Hussein, Dickson Job, Bakari Nondo Mwamyeto, Mzamiru Yassin, Salum Aboubakar/Mudathir, Feisal Salum, George Mpole/Jabir, Kibu Denis/Farid na Abdul Sopu
Soka Stars yaitoa Somalia CHAN
Stars yaitoa Somalia CHAN
Read also