Na mwandishi wetu
Timu ya Mbeya City imepokea kwa shauku kubwa ahadi ya shilingi milioni moja kwa kila ushindi wa mechi ya Ligi Kuu NBC, wakidhamiria kuvuna ahadi hiyo iliyowekwa na aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Ofisa Habari wa City, Shah Mjanja ameiambia GreenSports leo Jumatano kuwa ahadi hiyo imewaongezea morali kwenye mipango yao na kwamba wataendelea na mazoezi bila kupumzika katika kipindi hiki mpaka watakapocheza mechi yao inayofuata dhidi ya Kagera Sugar Aprili 23, mwaka huu.
Mbeya City inashikilia nafasi ya 13 kwa pointi 27 ikipambana isicheze mechi za mtoano kuwania kubaki Ligi Kuu NBC au kutoshuka daraja mwisho wa msimu huu.
“Tunamshukuru sana Sugu, hii motisha kwa nafasi yake itasaidia pia kukuza mpira na hii itaongeza motisha kwa timu maana tulianza vizuri lakini sasa tupo chini, kwa ahadi hii itaongeza chachu maradufu ya kupambana kwenye mechi hizi nne zilizobaki.
“Binafsi nimezungumza na Sugu na kumpongeza kwa kuongeza kitu kama hiki na timu kwa sasa itaendelea na mazoezi mpaka siku ya mchezo unaofuata dhidi ya Kagera Sugar, tumedhamiria kufanya vizuri kwa kweli na motisha imekuja wakati muafaka,” alisema Mjanja.
Soka Mbeya City waifurahia milioni ya Sugu
Mbeya City waifurahia milioni ya Sugu
Read also