Na mwandishi wetu
Hatimaye klabu ya Azam imetangaza rasmi kumsajili kiungo Yanick Bangala kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga SC.
Bangala aliyekuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo ya Jangwani, ametua Azam baada ya makubaliano ya klabu hizo mbili, ikielezwa ameuzwa kwa kitita cha Sh milioni 100.
Azam kupitia kurasa za mitandao yao ya kijamii, leo Jumamosi imemtangaza mchezaji huyo raia wa DR Congo (DRC), ikimkaribisha na kufafanua imekamilisha usajili huo baada ya kiungo huyo kufuzu vipimo vya afya.
“Tumefikia makubaliano na klabu ya Yanga ya kumnunua mchezaji kiraka, Yanick Bangala na amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya kufuzu vipimo vya afya. Bangala karibu Mbagala,” ilieleza taarifa hiyo.
Bangala aliyeibuka Mchezaji Bora wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2021-22, taarifa zake za kutua Azam zilianza kuvuma mapema baada ya kumalizika msimu wa 2022-23 kabla ya baadaye Yanga kutomtambulisha kwenye Siku ya Mwananchi na kuthibitisha uwepo wa taarifa hizo.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Bangala na beki wa kulia, Djuma Shaban walitaka kutolewa kwa mkopo Singida Fountain Gate lakini waligomea dili hilo.
Na baada ya kumchukua Bangala, Azam sasa inakuwa imenasa mchezaji wa pili kutoka Yanga katika dirisha hili kubwa la usajili baada ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye naye usajili wake ulikuwa wa vuta nikuvute.
Soka Bangala atua Azam FC
Bangala atua Azam FC
Read also