Na mwandishi wetu
Siku moja baada ya Ally Kamwe kutambulishwa kuwa ofisa habari mpya wa Yanga, ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa timu hiyo kuhakikisha wanamaliza changamoto walizonazo na kuipeleka timu mbali.
Ofisa huyo ametambulishwa usiku wa juzi, sanjari na Mtendaji Mkuu, Andre Mtine raia wa Zambia na Mkuu wa Kitengo cha Digitali na Maudhui, Priva Abiud.
Kamwe ambaye awali alikuwa mchambuzi wa Kituo cha Azam Media, kwanza ametanguliza shukran zake kwa uongozi, watendaji, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa kumpokea vizuri na kumpongeza tangu alipotangazwa kuchukua mikoba hiyo.
“Shukran kwa uongozi wa klabu na kamati ya utendaji chini ya Rais wetu, Hersi Said, ni imani kubwa kwangu wameionyesha na kwa tasnia ya habari kwa ujumla maana mimi ni mmoja kati ya vijana wengi wanaofanya kazi kwenye media na kama nimeaminika kwa taasisi kubwa kama Yanga basi ni jambo kubwa kwangu.
“Shukran kwa uongozi na mashabiki kwa mapenzi makubwa ambayo wamenionyesha tangu jana (juzi) tangu nimechaguliwa kumekuwa na simu, meseji nyingi za pongezi, niseme tu kwamba nawashukuru na nipo tayari kwa kazi,” alisema Kamwe.
Kamwe ambaye alifafanua kuwa kufanya kazi kwenye klabu kubwa kama Yanga lazima kuna changamoto zitakuwepo na yeye peke yake hawezi, hivyo atashirikiana na viongozi wa idara mbalimbali, wanachama na mashabiki wa Yanga kupambana na hizo changamoto za kuivusha Yanga kutoka ilipo sasa.
“Yanga ni kubwa Tanzania, chochote chenye ukubwa kina changamoto na mimi jukumu langu kubwa ni kushirikiana na viongozi, idara, wanachama na mashabiki kupambana na hizi changamoto, lengo letu ni kuiona Yanga inapiga hatua…
“Inatangazwa vizuri Afrika na duniani kwa ujumla, mimi na wenzangu kwa kushirikiana na wanachama na mashabiki tunayo nguvu ya pamoja ya kuivusha klabu yetu kuipeleka kwenye ‘level’ ya juu zaidi,” alisema Kamwe.
Pia upande wa Abiud aliyekuwa Kituo cha Redio cha Clouds naye alisema: “Hii imetupa imani kubwa na ni kama ujumbe kwa vijana wengine kuaminishwa kwamba hizi timu kubwa zinaamini katika kila nguvu na wanachohitaji kwetu ni kile tulichokuwa tukihubiri na sasa ni wakati wa kukifanyia kazi.”
Soka Ali Kamwe aahidi ushirikiano Yanga
Ali Kamwe aahidi ushirikiano Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
