Liverpool, England
Klabu ya Liverpool inadaiwa kuwasilisha rasmi maombi ya kufanya mazungumzo na kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso ikiamini ni mtu sahihi kumrithi kocha wa sasa wa timu hiyo, Jurgen Klopp.
Klopp ameshatangaza kwamba huu ni msimu wake wa mwisho na Liverpool, timu ambayo hivi karibuni ameipa taji la Carabao na tayari mabosi wa timu hiyo wameanza kumfikiria mtu wa kuziba nafasi hiyo.
Alonso, kiungo wa zamani wa Liverpool anabebwa na mafanikio yanayoonekana Leverkusen, timu ambayo kwa sasa inashika usukani katika Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga ikitishia himaya ya mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Bayern Munich.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari nchini Ujerumani, Liverpool imeweka nguvu kubwa kwa Alonso kwa kuzingatia historia yake na klabu hiyo ikiamini ni mtu sahihi kukabidhiwa majukumu ya Klopp.
Liverpool imeamua kuanza mbio hizo mapema licha ya kuamini kwamba ina nafasi kubwa ya kumpata kocha huyo kutokana na historia yake kwenye klabu hiyo aliyowahi kuichezea kati ya mwaka 2004 na 2009.
Klabu hiyo hata hivyo inatambua uwezekano wa Alonso kuwindwa kimya kimya kwingineko barani Ulaya, mfano Bayern Munich imetangaza kuachana na kocha wake wa sasa Thomas Tuchel ambaye huu ni msimu wake wa mwisho na haitokuwa ajabu Alonso akipewa nafasi hiyo.
Barcelona nayo imetangaza kuachana na kocha wake wa sasa Xavi ambaye naye huu utakuwa msimu wake wa mwisho, uwezekano wa Alonso kwenda Barca pia si jambo la kupuuza.
Kimataifa Liverpool yamuita Alonso mezani
Liverpool yamuita Alonso mezani
Read also