Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino amesema vituo vya Ufundi vya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kigamboni, Dar es Salaam na Mnyanjani, Tanga ni sehemu ya kuunganisha dunia.
Infantino alisema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF Kigamboni, Dar es Salaam, leo Jumamosi na kusema soka linaunganisha dunia hivyo vituo hivyo viwili vitakuwa sehemu ya kufundishia vijana soka linalounganisha dunia.
“Soka linaunganisha dunia, linaanzia hapa katika mradi huu mzuri wa Kigamboni na Tanga ambao ni sehemu inayowapa vijana wa kike na wa kiume fursa nyingi kwao, familia na nchi hivyo nafurahia kuona fedha zinazotolewa na Fifa zikifanya miradi ya maendeleo,” alisema Infantino.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka Duniani, Arsene Wenger alisema: “Pongezi kwa Tanzania kwa kazi inayofanywa na Rais Karia kwa kutengeneza kiwanja kizuri ambacho kitawapa nafasi vijana kucheza na mimi naahidi kurudi hapa.
“Tuko pamoja na Tanzania na naahidi kuweleta makocha hapa ambao watawafundisha vijana na kuwafundisha makocha namna ya kuchagua vijana na kuwapa nafasi ya kuonesha vipaji vyao.”
Infantino, Wenger, Pierluigi Collina ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Fifa, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrick Motsepe, Katibu Mkuu wa Caf, Veron Mosengo, Katibu Mkuu wa Fifa, Fatma Samoura, Mwakilishi Fifa Ukanda wa CECAFA, Andrea Silva na viongozi wengine waandamizi wa Fifa na Caf walikuwa nchini kwa ajili ya ufunguzi wa michuano ya African Football League (AFL) uliowakutanisha Simba SC dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kimataifa Infantino: Vituo vya TFF kuiunganisha dunia
Infantino: Vituo vya TFF kuiunganisha dunia
Read also