Budapest, Hungary
Paris St-Germain au PSG ya Ufaransa kwa mara ya pili mfululizo imedhihirisha ubora wake barani Ulaya kwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufuta matumaini ya Arsenal kubeba taji hilo.
PSG wamebeba taji hilo kwa ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Arsenal baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi iliyochezwa Jumamosi, Mei 30, 2026 mjini Budapest, Hungary.
Miezi 12 iliyopita, ni PSG hao hao waliolibeba taji hilo kwa kuichapa Inter Milan mabao 5-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa mjini Munich, Ujerumani.
Arsenal waliouanza vyema mchezo wakiwa na matumaini makubwa yaliyozaa bao la mapema dakika ya sita mfungaji akiwa ni Havertz kwa pasi ya Trossard, bao lililodumu kwa dakika 45 za awali.
PSG walipambana na kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Dembele katika dakika ya 65 kwa mkwaju wa penalti na hatimaye timu kumaliza dakika 90 kwa sare pamoja na 30 za nyongeza kabla ya kuingia kwenye penalti na PSG kuibuka mashujaa.
Furaha isiyo kifani ilidhihirika kwa kocha wa PSG, Luis Enrique anayeingia katika rekodi ya watu watano waliobeba taji hilo mara tatu na ambaye alinukuliwa baada ya mechi akisema kwamba amechanganywa kwa furaha.
“Nina furaha, uchovu wa akili na kila kitu lakini hili ni tukio muhimu la msimu, sisi bado ni mabingwa, mara mbili mfululizo, ni jambo la kipekee,” alisema Enrique.
Mtu mwingine aliyedhihirisha furaha ya ushindi huo ni rais wa klabu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi ambaye baada ya Enrique kuvalishwa medali yake, wawili hao walionekana wakicheza mbele ya mashabiki kufurahia taji hilo.
PSG chini ya Enrique ambaye pia alilibeba taji hilo mwaka 2015 akiwa mchezaji wa Barcelona, tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa timu hiyo Julai 2023 amefanikiwa kuigeuza kuwa timu bora.
Baada ya kuachana na baadhi ya wachezaji mastaa kina Lionel Messi, Kylian Mbappe, Neymar Jr na wengineo, Enrique ni kama alianza kufanya kazi ya kuisuka upya PSG na akafanikiwa kuifanya iwe katika ubora.
Ubora wa timu hiyo ukiendelea hakuna atakayeshangaa iwapo wataisogelea rekodi ya Real Madrid ya kutwaa mataji matano ya Ulaya kwa miaka mitano mfululizo waliyoiweka kati ya mwaka 1956 hadi 1960.
Kimataifa PSG yabeba tena taji Ulaya
PSG yabeba tena taji Ulaya
Read also
