Na mwandishi wetu
Leo jioni Pamba inacheza na Simba katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Azam, wakati ikiwa katika maandalizi ya mechi hiyo muhimu imemtimua kocha wake, Wilbert Mweta. Kutimuliwa kwa kocha huyo kuliibua sintofahamu lakini leo kocha huyo ameibuka akidai kwamba sababu hasa ya kutimuliwa kwake ni uamuzi wake wa kutowasikiliza viongozi wa timu.
Juzi wakati, Pamba ikiendelea na maandalizi ya mechi hiyo, kukawa na taarifa kuwa timu hiyo imemtema kocha wake huku ikielezwa kuwa sababu za kufanya hivyo zitawekwa wazi baadaye.
Mweta amefafanua kuwa aliitwa ghafla juzi na kuambiwa amefutwa kazi kwa sababu ya kutosikiliza viongozi wake, hivyo ikabidi akamilishe taratibu nyingine za kuiacha timu siku hiyo hiyo na kuendelea na shughuli zake nyingine huku akiamini misimamo yake katika kazi ndiyo imemponza.
“Baada ya kuniita waliniambia kwamba sitaendelea tena kuinoa timu kwa kuwa wameniondoa na sababu kubwa ni kwamba sisikilizi viongozi, basi nikaona mambo ni mengi ukitazama na jinsi ilivyokuwa, nikaona misimamo yangu ya kazi kama kocha imeniponza, sikuwa napenda kuingiliwa katika kazi na nilihitaji kila kitu kikae kwenye mstari wake.
“Nilikuwa nimeitoa timu mbali tangu nilipoichukua na kuisogeza nafasi za katikati, nimefanikiwa kufika robo fainali Kombe la FA (Azam) na nilitaka kuendelea na huu mchakato wa kuifikisha timu mbali kwenye michuano hiyo lakini imekuwa tofauti,” alisema Mweta aliyekuwa akikaimu nafasi ya kocha mkuu Athumani Cairo aliyetimuliwa.
Mweta amedumu katika kikosi cha timu hiyo ya Mwanza kwa takribani miezi mitano baada ya kupokea mikoba ya kuinoa timu hiyo Januari, mwaka huu.
Kwa upande wao Pamba wamesema kuwa kufutwa kazi kwa Mweta aliyekuwa akikaimu nafasi ya Cairo hakuhusiani na lolote kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba huku akisisitiza kuwa sababu za kuachana na Mweta zitawekwa wazi hivi karibuni.
Mweta aliyedumu na timu hiyo takriban miezi mitano alipewa nafasi hiyo baada ya kuondolewa kwa Cairo aliyedumu klabuni hapo kwa mwezi mmoja na siku 17 tangu alipojiunga nayo akitokea Mbao FC.
“Ni kweli kikawaida unawezekana ukajiuliza kwamba imekuwaje siku moja kabla ya mechi na Simba lakini itakuwa imekuwa hivyo kwa sababu ni Simba tu, sidhani kama ingeshtua sana kama ingekuwa ni timu nyingine, lakini sikatai wapo sahihi kufikiria hivyo pia kibinadamu.
“Lakini niseme pengine imetimia katika siku ambayo sisi kesho (leo) tuna mchezo ila ilikuwa iko hivyo. Kuhusu sababu tutaziweka wazi muda si mrefu lakini itoshe kusema tulikaa na kocha na kuafikiana kwa maslahi ya timu inabidi tuchukue hatua hii na timu kuwa chini ya Yangoo Mamboleo wakati tukiendelea na taratibu nyingine,” alisema William.
Pamba inayoshiriki Ligi ya Championship inashikilia nafasi ya tisa ikiwa na pointi 36 zikiwa zimesalia mechi mbili kabla ya kuisha kwa ligi.
Habari nyingine za ndani zinadai kuwa matokeo mabaya ya timu hiyo ndio chanzo cha kuondolewa kwa kocha huyo kwani kwa sasa Pamba inapambana kushinda mechi zake mbili zilizobaki ili isimalize chini ya nafasi ya 10 na kucheza play-off kuwania kusalia kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Soka Kocha Pamba ataja kilichomtimua
Kocha Pamba ataja kilichomtimua
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
