Na mwandishi wetu
Hatua ya TFF kuahirisha tuzo zake za kila mwaka imeonekana kuwachukiza baadhi ya mashabiki na wadau wa soka ambao wametumia mitandao ya kijamii kueleza hisia zao.
Kwa mujibu wa mapitio ya kwenye mitandao ya kijamii yaliyofanywa na GreenSports, wadau walio wengi hawaungi mkono uamuzi huo na kutoa maoni ya kutofurahishwa na shirikisho hilo.
Uamuzi wa TFF ulitangazwa Jumatano hii kupitia taarifa maalum ya shirikisho hilo iliyosainiwa na ofisa habari na mawasiliano, Cliford Ndimbo imeeleza kuwa tuzo hizo sasa zitafanyika wakati wa michezo ya Ngao ya Jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF lengo la uamuzi huo ni kufanya tukio la utoaji tuzo hizo kuwa bora zaidi na kukidhi malengo ya mahitaji yake.
Kutokana na mabadiliko hayo, tuzo za msimu wa 2023-24 uliofikia tamati Jumanne iliyopita ambazo zilitakiwa kutolewa katika siku za karibuni, sasa zitatolewa wakati wa mechi za Ngao ya Jamii za kuukaribisha msimu mpya wa 2024-25.
Kwa kawaida tuzo hizo zinazoandaliwa na TFF kwa ushirikiano na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) huwatunuku zawadi wanamichezo waliofanya vizuri katika msimu uliomalizika.
Baadhi ya wadau wameona kama uamuzi huo utazipoozesha tuzo hizo na kuzifanya zisiwe na hamasa kama inavyotakiwa.
“Wanasema tuzo zitakuwa bora zaidi na kukidhi malengo hapo hapo hawafafanui kivipi, sasa tueleweje,” ilisomeka taarifa ya mdau mmoja kupitia mtandao wa Facebook.
Mbali na mdau huyo, kwa mujibu wa mapitio ya GreenSports, wadau wengine wanaona kama TFF imefanya uamuzi unaokwenda kinyume na kanuni na taratibu zilizowekwa na wao wenyewe ambazo ndizo zinazosimamia uendeshaji wa tuzo hizo.
