Manchester, England
Beki wa kati ya timu ya Taifa ya Ufaransa na klabu ya Manchester United, Raphael Varane ametangaza kustaafu kuichezea timu yake ya Taifa.
Varane (pichani) ambaye alikuwa na kikosi cha timu ya Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi, anastaafu akiwa ameifungia Ufaransa mabao matano katika mechi 93 tangu aichezee timu hiyo mara ya kwanza mwaka 2013.
Anakuwa mchezaji wa pili wa Ufaransa kustaafu timu ya Taifa kwa siku za karibuni akiwa ametanguliwa na kipa na aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Hugo Lloris ambaye alitangaza kutaafu mwezi uliopita.
Mara ya mwisho, Varane alikuwa na kikosi cha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022 ingawa walishindwa kutamba mbele ya Argentina waliobeba taji wakiilaza Ufaransa kwa penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 3-3 katika dakika 120.
Varane anajivunia kuiwakilisha Ufaransa kwa kipindi kirefu hadi sasa anaamua kustaafu “Kuiwakilisha nchi yetu kwa muongo mmoja (miaka 10) ni moja ya heshima kubwa katika maisha yangu.”
“Kila wakati nikivaa jezi hii ya kipekee ya bluu naona ufahari wa aina yake, wajibu wa kujitoa kwa kila kitu, kucheza nikiuridhisha moyo wangu na kushinda kila wakati ninapokuwa uwanjani,” alisema Varane.
“Nimekuwa nikilitafakari jambo hilo kwa miezi kadhaa sasa na hatimaye kuamua kwamba huu ni wakati sahihi kwangu kustaafu soka la kimataifa,” aliongeza.
Varane ambaye alikuwa akitajwatajwa kuwa mrithi wa Lloris katika nafasi ya unahodha wa timu hiyo, moja ya kumbukumbu zake kubwa za utotoni ni wachezaji mastaa waliokuwa na timu ya Ufaransa iliyobeba taji la dunia mwaka 1998 nchini Ufaransa.
“Nikiwa mdogo nakumbuka kuifuatilia timu ya Ufaransa ya mwaka 1998, wachezaji hawa walitupa uzoefu na mvuto wa kipekee,” alisema.
“Nilijiwa na ndoto za kuwa shujaa na miaka 20 baadaye niliishi ndoto hiyo na kujikuta katika tukio la kipekee katika maisha yangu, tukio ambalo limenifanya nijivunie hasa, tulipeleka nyumbani Kombe la Dunia,” alisema.
“Kamwe sitokaa nisahau, bado nakumbuka mvuto na hamasa ya siku hiyo ya Julai 15, 2018, lilikuwa ni tukio la aina yake na la kuendelea kukumbukwa katika maisha yangu,” aliongeza Varane ambaye alijiunga na Man United Agosti 2021 akitokea Real Madrid.