Na mwandishi wetu
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) na Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania (IPRT) wamesaini makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuwajengea uwezo zaidi waandishii wa habari za michezo.
Katika makubaliano hayo, taasisi hizo mbili zinalenda kuandaa mafunzo ya mawasiliano kwa waandishi wa habari za michezo ili kuwajengea uwezo zaidi kuelekea mkakati wa pamoja wa taasisi hizo katika kukuza na kuendeleza michezo nchini.
Tukio la kusaini Mkataba wa Ushirikiano (MoU) limefanyika leo Alhamisi jijini Dar es Salaam likihusisha viongozi waandamizi wa taasisi hizo mbili akiwemo Mkurugenzi wa IPRT William Kallaghe, viongozi wa Taswa wakiongozwa na mwenyekiti wao, Amir Mhando, wadau wa michezo na waandishi wa habari.
Mafunzo hayo yatajumuisha maeneo manne ambayo ni mafunzo maalum ya mawasiliano na uongozi na mafunzo ya wazi ya mawasiliano na uongozi.
Mafunzo mengine ni ya waandishi wa habari za michezo ambayo pia yatahusisha waandishi waandamizi na mafunzo ya uwezeshaji waandishi wa habari za michezo wanawake.
Akizungumza katika mkutano huo, Kallaghe alisema ushirikiano wa Taswa na IPRT unawakilisha hatua muhimu katika kutumia nguvu za mawasiliano yenye ufanisi na uongozi thabiti katika kufanikisha ukuaji na maendeleo ya michezo nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Taswa, Alfred Lucas alisema wanafurahia kuungana na IPRT katika kufanikisha mkakati ambao utatoa fursa za kipekee kwa waandishi wa habari za michezo kujiongezea maarifa.
Sports Mix Taswa, IPRT kuwanoa waandishi
Taswa, IPRT kuwanoa waandishi
Read also