Dortmund, Ujerumani
Winga wa Man United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho hatimaye amerudi katika klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund ambayo imemsajili kwa mkopo kwa kipindi kilichobaki cha msimu wa 2023-24.
Sancho, 23, alijiunga na Man United, Julai 2021 akitokea Dortmund kwa ada ya Pauni 73 milioni lakini tangu Agosti mwaka jana amekuwa katika wakati mgumu baada ya kutofautiana na kocha wake, Erik ten Hag.
Tangu kutokea utata huo, Sancho alijikuta akiondolewa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo mwezi Septemba baada ya kutoa kauli ya kumpinga kocha wake kwenye mitandao ya kijamii.
“Nilipokuja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo leo, nilijiona kama nakuja nyumbani, naijua hii klabu nje ndani, wakati wote nimekuwa karibu na mashabiki wa hapa na sijawahi kukosa mawasiliano na wenye mamlaka,” alisema Sancho.
Sancho amekuwa na Dortmund tangu mwaka 2017 na kuifungia mabao 50 katika mechi 137 kabla ya kusajiliwa na Man United mwaka 2021.
Utata wa Sancho na Dortmund ulianza kuibuka baada ya Man United kupoteza mechi na Arsenal ambapo Ten Hag alisema kwamba hakumpa nafasi mchezaji huyo kwa sababu alizembea mazoezini.
Sancho ambaye anaondoka Man United akiwa na mabao 12 katika mechi 87, alimpinga Ten Hag kupitia mitandao ya kijamii akidai kwamba kocha huyo hakuwa mkweli na kauli yake ilikuwa ya kumtoa kafara.