Na mwandishi wetu
Baada ya kikosi cha Yanga kutua nchini Misri kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema wamejipanga kuonesha kiwango bora zaidi ya ilivyokuwa katika mchezo wao na CR Belouizdad.
Jumamosi iliyopita Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Belouizdad ya Algeria kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku wakionesha kiwango cha hali ya juu na kuwavuruga wapinzani wao.
Akizungumza na mtandao wa klabu hiyo kuelekea mchezo wao dhidi ya vinara hao wa kundi lao na mabingwa watetezi wa taji hilo, Gamondi alisema dhamira yao ni kumaliza vinara wa kundi lakini pia kucheza kwa kufuata falsafa zake ambazo ni kucheza kwa kiwango kikubwa zaidi ya ilivyokuwa mchezo uliopita.
“Nimewaambia wachezaji wangu tunatakiwa kucheza kama vile hatujavuka hatua ya robo fainali, lengo ni kupata ushindi na kumaliza wa kwanza kwenye kundi lakini pia tunapaswa kuonesha ubora mara mbili zaidi ya ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita sababu hiyo ndio falsafa yangu,” alisema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo utakaochezwa kesho Ijumaa saa moja usiku, Uwanja wa Cairo International yanakwenda vizuri na amewaandaa wachezaji wake vizuri kuhakikisha wanamaliza kwa heshima hatua hiyo ya makundi.
Timu zote mbili tayari zimekata tiketi ya kucheza robo fainali, Ahly ikiwa na pointi tisa huku Yanga ikiwa ya pili kwa pointi zao nane hivyo mchezo huo utakuwa wa kukamilisha ratiba na kuweka heshima.