Na mwandishi wetu
Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (pichani) amemmwagia sifa kiungo wa timu hiyo, Clatous Chama kwa kuonesha thamani yake halisi kwa mabao aliyofunga katika sare ya 2-2 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, Jumamosi iliyopita.
Simba ilipata sare hiyo kwenye mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola na Chama raia wa Zambia kufunga mabao yote mawili.
Tshabalala au Zimbwe Jr, alisema kitendo cha Chama kufunga mabao hayo katika ardhi ya nyumbani kwao kimeonesha thamani yake kwa klabu na taifa lake kulingana na kiwango kikubwa alichokionesha pia.
“Nimefurahi sana kuona Chama akifanya kitu kikubwa na kuoneha thamani yake kwa klabu na taifa lake, ameenda kama mchezaji wa taifa lile na kuipatia mabao timu yake katika ardhi ya nyumbani, ameonesha pia umuhimu wa Simba kumuamini na kusaidia timu kupata matokeo,” alisema Tshabalala.
Beki huyo wa kushoto pia alisema kwamba hakutegemea kama wangepata sare katika mchezo huo kulingana na nafasi walizotengeneza lakini ni matokeo ya mpira na mwisho wanajifunza kwa yaliyotokea.
Wekundu hao watarudiana na Dynamos Oktoba Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wakihitaji matokeo ya suluhu, sare ya bao 1-1 au ushindi wowote kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Soka Tshabalala ampongeza Chama
Tshabalala ampongeza Chama
Read also