Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji mpya wa timu ya Simba, Aubin Kramo amesema kilichomshawishi ajiunge na timu hiyo ni rekodi nzuri kwenye mashindano ya kimataifa.
Kramo amejiunga na miamba hiyo ya soka kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyofika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
Akizungumza na mtandao wa klabu hiyo, mchezaji huyo mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kufunga mabao alisema malengo yake ni kucheza timu yenye mikakati ya kushiriki mashindano makubwa na kubeba mataji ya Afrika na anaamini Simba ndio sehemu sahihi ya kutimiza ndoto zake.
“Nilikuwa na ofa za kwenda Raja Casablanca (Morocco) na Esperance ya Tunisia lakini niliichagua Simba, kutokana na kuvutiwa na mikakati waliyokuwa nayo hasa kwenye mashindano ya kimataifa, siku zote huwa napenda kushinda mataji,” alisema Kramo.
Kiungo huyo alisema baada ya dili lake la kujiunga na Simba, mipango yake ni kuhakikisha anapambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili kufikia malengo ya klabu kwenye mashindano yote ambayo watashiriki msimu unaokuja.
Alisema anajua Simba imesajili wachezaji wazuri na wenye majina makubwa lakini na yeye atapambana kuhakikisha anaonesha kitu cha tofauti ambacho kitamwingiza kwenye orodha ya wachezaji walioifanyia kitu timu hiyo.
Kramo ni miongoni mwa wachezaji waliotamba kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita akiwa na Asec ikiwemo kufunga mabao manne kitu ambacho kiliwavutia viongozi wa Simba na kuamua kumsajili.