Frankfurt, Ujerumani
Mshambuliaji wa timu ya Eintracht Frankfurt, Randal Kolo Muani (pichani) amekwepa kufanya mazoezi ya timu hiyo leo Jumatano ikiwa ni mkakati wa kulazimisha kuhama ili ajiunge na PSG.
Habari zaidi zinadai kwamba mshambuliaji huyo Mfaransa tayari yuko Paris, Ufaransa yalipo makao makuu ya klabu ya PSG ambayo inahaha kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.
PSG imeondokewa na Lionel Messi aliyetimkia nchini Marekani katika klabu ya Inter Miami pamoja na Neymar ambaye hivi karibuni alijiunga na klabu tajiri ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Kolo Muani alishaweka wazi mpango wake huo mapema alipozungumza na chombo kimoja cha habari na kusema kwamba anataka kuhamia PSG.
“Mshambuliaji Randal Kolo Muani leo (Jumatano) ameuarifu uongozi wa klabu ya Eintracht Frankfurt kuwa hatofanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi ya Alhamisi ya Europa Conference Ligi dhidi ya Levski Sofia,” ilieleza taarifa ya Frankfurt.
“Amebainisha wazi azma yake ya kutaka kubadili klabu kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Ijumaa usiku kuwa hiyo ndiyo sababu ya yeye kukosekana.”
Frankfurt bado inamhitaji mshambuliaji huyo ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea Nantes ya Ufaransa na msimu uliopita ulikuwa na mafanikio kwake akifunga mabao 23 katika mechi 46 za mashindano tofauti na tayari ameuanza msimu huu na mabao matatu katika mechi nne.
Uamuzi wake wa kususia mazoezi umemkera mjumbe wa bodi ya klabu ya Frankfurt, Markus Krosche ambaye amesema kwamba huyu si Randal waliyemjua na wanayezijua vizuri tabia zake.
Mpango wa mchezaji huyo ambaye ameifungia timu ya taifa ya Ufaransa bao moja katika mechi tisa ukifanikiwa, akiwa PSG ataungana na nyota wenzake wa Ufaransa Kylian Mbappe na Ousmane Dembele.
Akiwa na timu ya Ufaransa mwaka jana kwenye fainali Kombe la Dunia, Kolo Muani anakumbukwa kutoa mchango mkubwa alipoingia katika mechi ya fainali dhidi ya Argentina, mechi ambayo iliisha kwa sare ya mabao 3-3 kabla ya Ufaransa kukwama kwenye mikwaju ya penalti.