Riyadh, Saudi Arabia
Mshambuliaji wa Paris Saint Germain (PSG), Lionel Messi anatarajia kuhamia Saudi Arabia na kujiunga na klabu ya Al Hilal ambao ni mahasimu wakuu wa klabu ya Al Nassr anayochezea Cristiano Ronaldo.
Mkataba wa Messi na PSG unafikia ukomo baadaye mwaka huu majira ya kiangazi lakini hadi sasa hajaonyesha nia yoyote ya kuongeza mkataba huku habari za ndani zikidai tayari ameanza mazungumzo na klabu hiyo ya Saudi Arabia.
Vigogo wa klabu ya Al Hilal inadaiwa wameweka mkazo katika mpango mzima wa kumshawishi mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona ili amfuate Ronaldo katika jiji la Riyadh.
Messi mwenye umri wa miaka 35 ambaye anaendesha kampeni za kutangaza utalii nchini Saudi Arabia pia inadaiwa ameshawekewa ofa mezani kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo.
Habari nyingine zinadai kwamba hadi juzi Jumanne, Messi aliyetua PSG mwaka 2021 akitokea Barca, hakuonyesha dalili za kuongeza mkataba na PSG jambo linalozipa nguvu habari za kuelekea Riyadh.
Kwa upande mwingine, mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na mipango ya kurudi Hispania na kujiunga na Barca huku rais wa klabu hiyo, Joan Laporta akihaha kufadhili mpango huo.
Barca hata hivyo inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na hivyo huenda hali hiyo ikawa kikwazo kwa mchezaji huyo kujiunga na timu hiyo kwa mara nyingine.
Messi pia anadaiwa kuwa katika mazungumzo na klabu ya Inter Miami ya Marekani lakini huenda kukawa na ugumu kwa klabu hiyo kumpata kwani haitokuwa tayari kushindana na ofa itakayowekwa mezani na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Al Hilal kwa sasa inanolewa na mshambuliaji wa zamani wa Argentina, Ramon Diaz, na ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Saudi Arabia lakini pia ni kati ya timu zenye mafanikio makubwa katika Ligi ya Mabingwa Asia.
Inadaiwa kwamba Saudi Arabia inafanya kila linalowezekana kuinua na kulipa umaarufu soka la nchi hiyo na uwapo wa Messi na Ronaldo unaweza kuwa na faida kubwa katika mpango huo.
Saudi Arabia pia inajipanga kuwania kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia baada ya mafanikio yaliyoonekana Qatar ambao walikuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa mafanikio makubwa.
Mpango huo wa Saudi Arabia unafanyiwa kazi katika namna mbalimbali mojawapo ikiwa ni mkakati maalum wa kusajili wachezaji mastaa wenye majina makubwa.
Kimataifa Messi kumfuata Ronaldo Saudia
Messi kumfuata Ronaldo Saudia
Read also