na mwandishi wetu
Sare dhidi ya Tanzania Prisons imeibua hofu miongoni mwa mashabiki wa
Yanga, baada ya matokeo ya mechi hiyo ya Jumatatu usiku, mashabiki
walianza kutoa lawama zao.
Ukweli kwamba Yanga ndiyo inayoongoza ligi tena kwa tofauti kubwa tu
ya pointi haujatosha kuwatuliza mashabiki hao na kujenga imani kwamba
Yanga bado wana nafasi, tena kubwa tu ya kulibeba taji la Ligi Kuu NBC
Bara msimu huu.
Na huo ndio ukweli, tukiulizana na kuweka unazi na hofu kando ni timu
gani yenye nafasi kubwa ya kutwaa taji msimu huu, haihitaji utafiti wa
aina yoyote, bila wasiwasi jibu ni Yanga.
Ukweli huo unabebwa na namba, Yanga ndio wanaoongoza ligi wakiwa na
pointi 57 katika mechi 23 walizocheza wakifuatiwa na Simba wenye
pointi 46 katika mechi 22.
Kinachowapa hofu zaidi mashabiki wa Yanga ni Simba kwamba inaweza
kupindua meza na kuweka rekodi ya kutwaa taji la tano la ligi hiyo
mfululizo na kuiacha Yanga katika nafasi ya pili.
Kimsingi Yanga hawahitaji na wala hawatakiwi kuwa na hofu na kuteseka
kwamba Simba wanaweza kupindua meza badala yake wanapaswa kuamini
kwamba wana timu nzuri ya kumalizia kazi iliyobaki kabla ya kutawazwa
mabingwa wa ligi msimu wa 2021/22.
Mashabiki wa Yanga wameshitushwa na matokeo ya sare mfululizo ambayo
timu yao imeyapata katika mechi za hivi karibuni, ikianzia mechi ya
Simba ambayo timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana, matokeo haya
hayakuibua hofu bali mijadala ilijaa majigambo na mabishano kuhusu
wachezaji na ubora au udhaifu wa kila timu.
Yanga baada ya matokeo haya walijiona wako juu na hakuna wa kuwazuia
hasa baada ya Simba nayo kushindwa kupata faida ya pointi tatu katika
mechi hii, pointi ambazo walau zingeonyesha dhamira yao ya kuikimbilia
Yanga katika mbio za kulisaka taji la ligi.
Baada ya hapo ikaja mechi dhidi ya Ruvu Shooting ambayo nayo matokeo
yalikuwa sare ya bila kufungana, hii ikaanza kuleta dalili ambazo si
nzuri, taratibu hofu ikaanza kujengeka, hofu ambayo ni kama vile
imeongezwa nguvu na sare nyingine dhidi ya Prisons.
Baada ya mechi na Prisons, lawama zilianza kurushwa kwa wachezaji
kushindwa kutumia nafasi walizotengeneza, Fiston Mayele kwa kukosa
penalti, Makambo kushindwa kuitumia vizuri pasi ya Mayele, Fei Toto
kwa kutofunga akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga na badala yake
kumpa Mayele ambaye alishindwa kuitumia nafasi hiyo na mengineyo.
Kwanza ni lazima mashabiki wafahamu kwamba Ligi ya NBC sasa imefika
pagumu, kuna timu chache zinapambana au zinawaza uwezekano wa kuipiku
Yanga na kutwaa taji lakini zipo nyingi zilizopoteza matumaini hayo na
badala yake zinapambana kujinasua na janga la kushuka daraja.
Prisons ni moja ya timu zinazopambana kujinasua za janga hilo, namba
haziongopi katika hilo, hali ni hiyo hiyo kwa Ruvu ambayo nayo
inapambana ama kushinda au kuambulia japo pointi moja itakayokuwa na
manufaa mbele ya safari kuliko kupoteza kabisa mchezo na hivyo
kujiweka katika mazingira magumu ya kujinasua mkiani.
Kwa kujua ugumu wa mechi yao na Yanga kwamba kuifunga ni kazi ngumu,
ndiyo maana Prisons walionekana kabisa kucheza kwa kujihami zaidi
wakati Yanga wakipambana kusaka bao. Prisons walifanikiwa katika
mpango wao na Yanga walikwama.
Ni hivyo hivyo pia kwa Ruvu, walifanikiwa na Yanga wakakwama, hata
hivyo Yanga hawajakwama katika mbio za ubingwa, bado wana nafasi ya
kurekebisha makosa na kufanya vizuri katika mechi zijazo, uwezo huo
wanao na wengi wetu tunaamini ndivyo itakavyokuwa na la muhimu zaidi
ni kwamba Yanga hawajabweteka, wanapambana.
Ukiangalia tukio la Mayele na Fei Toto, ukweli ni kwamba mwenye uwezo
zaidi wa kufunga katika Yanga ni Mayele, haishangazi anapopewa mipira
mingi ingawa ni Fei Toto anayeweza kulizungumzia zaidi hilo kwamba kwa
nini hakufunga na badala yake akampasia Mayele.
Malalamiko mengine yakawa kwenye penalti, kwa nini hakupiga Djuma
Shabani na badala yake akapiga Mayele ambaye alikosa, tukio hilo
limepata nguvu hasa baada ya kuonekana Djuma akitaka kupiga penalti
ile lakini Mayele naye akaitaka na hivyo akaachiwa.
Sababu ya kumtaka Djuma apige penalti hiyo ipo wazi kwamba ndiye
mpigaji penalti anayeaminika zaidi lakini pia tusisahau kwamba kwenye
penalti kuna suala la kujiamini, Mayele hadi anang’ang’ania kupiga
penalti maana yake alijiamini lakini pia anatafuta rekodi ya mabao 12,
anataka awe mfungaji bora, na kwa wachezaji walio wengi penalti ni
fursa ya kufunga, haishangazi kwa Mayele kuiona fursa hiyo na
kuikimbilia kwa haraka.
Hapa pia tunaweza kukumbushana tukio la mwaka 2010 kati ya wachezaji
Frank Lampard wa Chelsea na Didier Drogba katika mechi dhidi ya Wigan.
Chelsea walipata penalti na Drogba akataka apewe apige yeye badala ya
Lampard ambaye ndiye aliyekuwa akiaminika zaidi katika penalti kwenye
timu hiyo.
Drogba alitaka kupiga penalti ile kwa sababu alijiamini anaweza
kufunga lakini pia alikuwa akipambana katika mbio za kuwa mfungaji
bora dhidi ya Wayne Rooney wa Manchester United wote wakiwa na mabao
26.
Lampard alifunga penalti ile na baada ya mechi Drogba alipoulizwa
akasema kwamba Lampard alikuwa sahihi lakini hiyo ni baada ya yeye
kufunga katika dakika 90 za mchezo na kuibuka mfungaji bora wa ligi
akimbwaga Rooney. Ingetokea Lampard kukosa na Drogba azidiwe na Rooney
kwenye mabao pengine hali ingekuwa tofauti, Drogba asingesema
alichokisema.
Utaona tukio hilo linafanana kidogo na lile la Mayele tofauti ni
kwamba Chelsea walipata baada ya mpiga penalti tegemeo kupiga na Yanga
mpigaji tegemeo hakupewa nafasi lakini katika matukio yote kulikuwa na
suala zima la mchezaji kujiamini, ndivyo alivyofanya Mayele,
alijiamini lakini bahati haikuwa yake, alionyesha ufundi kwa kumpoteza
kipa lakini mpira alioupiga ulipaa.
Yote kwa yote, mashabiki Yanga hawana sababu ya kuhofia kuukosa
ubingwa, kwanza timu yao iko juu, inabebwa na namba, pia wana timu
nzuri ya kupambana na kupata matokeo katika mechi za ligi hii lakini
la mwisho ambalo ni muhimu ni kwamba wachezaji au timu haionyeshi
kubweteka, inapambana.
Wanachotakiwa kufanya mashabiki wa Yanga ni kusubiri, huenda kabla ya
mwisho wa mwezi huu wakatangazwa mabingwa msimu wa 2021/22. Ni suala
la muda mdogo ujao.
Soka Hofu ya ubingwa inawatesa Yanga
Hofu ya ubingwa inawatesa Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
