Na mwandishi wetu
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kukutana ulingoni, bondia Muller Junior amemweleza mpinzani wake Karim Mandonga (pichani) kuwa asitarajie ushindi kupitia umaarufu wake kwani atamchakaza vibaya.
Muller atamvaa Mandonga katika pambano la awali litakalopigwa Agosti 27, mwaka huu visiwani Zanzibar kabla ya pambano la ‘main card’ la Ibrahim Mgenda ‘Class’ dhidi ya Khamis Muathai.
Muller alisema kuwa amejiandaa vilivyo na ameshamaliza mazoezi, kwa sasa anamsubiri Mandonga ambaye hamuhofii akitamba anafahamu ni mtu maarufu lakini hawezi kumshinda siku hiyo.
“Hapa tulipo maandalizi yamekwisha, kwa sasa tunarashiarashia tu, nasema yeye (Mandonga) ni bondia maarufu lakini sio mkubwa, afanye afanyavyo lakini kipigo kipo palepale. Siwezi kumtabiria nitamchapa raundi ya ngapi lakini yeye si anajiamini basi tutaonana,” alisema Muller.
Mbali ya pambano hilo, pambano jingine la utangulizi linalotarajia kupigwa siku hiyo kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung litawakutanisha Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ dhidi ya Banja Hamisi.