Na mwandishi wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Nadumbaro (pichani) amesema hawatakuwa na msamaha kwa wanaojihusisha na utengenezaji jezi feki nchini kwa kuwa ni kati ya watu wanaozorotesha uchumi wa nchi nzima.
Ndumbaro ameyasema hayo ikiwa ni siku chache zimepita tangu kuelezwa kukamatwa kwa jezi bandia za Simba, Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars maeneo ya Chang’ombe na Temeke, Dar es Salaam zinazokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni mbili.
“Kama wizara kwanza tumesikitishwa sana na vitendo vya uharamia uliofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi yetu, tufahamu kwamba kutengeneza bidhaa bandia kwanza unaathiri uchumi wa nchi, unakiuka sheria za ushindani, hakimiliki na nembo pia, mbaya zaidi unaathiri uchumi wa nchi, klabu na sekta ya michezo kwa ujumla,” alisema Ndumbaro.
Waziri huyo alisema vitendo hivyo pia vinarudisha nyuma juhudi za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye anajipambanua kuinyanyua michezo nchini ili klabu ziwe na fedha na mapato mazuri ya kuendeleza michezo kwa manufaa ya uchumi wa nchi.
Alisema pamoja na mambo mengine lakini faida muhimu katika michezo ni ajira, biashara na uchumi, hivyo anayejaribu kuchezea vitu hivyo vitatu watamchukulia hatua stahiki ili watambue kwamba mali za klabu, mali za mpira sio vitu vya kuvichezeachezea.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji kwa kuwa masuala ya ushindani wa haki yako chini ya dhamana yake, tayari ameshachukua hatua, anaendelea na hatua za mwisho ili haki itendeke,” alisema Dk Ndumbaro.
“Na sisi Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tunamuunga mkono Kijaji, tunamuahidi kushirikiana naye kupigania haki na maslahi ya klabu za Tanzania na timu za taifa na kuhakikisha yeyote anayefanya uharamia katika jezi, nembo na vifaa vingine vya klabu atachukuliwa hatua stahiki, kwenye hili hatuna mchezo ili wajue mali za klabu, mali za mpira sio vya mchezo mchezo,” alisema Ndumbaro.