Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Yusuf Chippo amesema wameumia kupoteza mechi yao dhidi ya Dodoma Jiji na sasa wanarejea kujipanga kwa nguvu kuhakikisha wanapata matokeo kwenye mechi inayofuata dhidi ya Simba SC.
Coastal jana ilikubali kuchapwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kuandika kipigo cha nne mfululizo msimu huu.
Chippo alisema kuwa walijitahidi kupambana kuhakikisha wanapata matokeo kwenye mechi hiyo lakini hali imekuwa tofauti kutokana na makosa madogo yaliyofanywa na mabeki wao na sasa wanarejea kujipanga upya.
“Tumepoteza hii mechi ni kitu cha kuumiza lakini tutajitahidi tujipange tuangalie mechi ya Jumamosi na Simba tuone itakavyokuwa, mechi zote ni muhimu zina pointi tatu kwa hiyo tunaamini tutakaa chini turekebishe halafu turudi kupambana Jumamosi.
“Hata hivyo, ligi inaonesha ni ngumu maana ni mechi ya nne tunapoteza kwa mpigo, inatuwia vigumu sana kwetu hivyo tutajipanga turudi katika njia ya kuhakikisha tunapata pointi,” alisema Chippo raia wa Kenya.
Naye kocha msaidizi wa Dodoma, Kassim Liogope alieleza kuwa mechi hiyo ilikuwa ngumu kwa pande zote kutokana na ubora wa vikosi na mbinu walizokuwa nazo lakini mwisho wanashukuru hesabu zao kufanya kazi na kuondoka na ushindi.
“Mechi ilikuwa ngumu ina ushindani mkubwa kutokana na kufanana kwa aina ya soka na ubora kwa timu hizi, mbinu zilitumika nyingi sana na kila wakati ililazimika kufanya hivyo kutokana na mbinu za Dodoma lakini tunashukuru mwisho tumepambana na tumepata matokeo na tunashukuru wachezaji kwa kujituma kwao na kupata ushindi,” alisema Liogope.
Soka Kipigo chamuumiza kocha Coastal
Kipigo chamuumiza kocha Coastal
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
