Naples, Italia
Kocha wa England, Gareth Southgate amesema timu yake inatakiwa kutumia tukio la Italia kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 kama onyo kwao kutoamini watafuzu kiulaini Euro 2024.
Italia ilibeba taji la Euro 2020 kwa kuifunga England kwenye penalti lakini haikufuzu fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar mwaka jana baada ya kushindwa kutamba mbele ya North Macedonia.
Katika kuwania kufuzu Euro 2024, England ipo Kundi C ambalo mbali na Italia pia lina timu za North Macedonia, Malta na Ukraine na itaanza kurusha karata yake dhidi ya Italia hii leo Alhamisi ikisaka ushindi wa kwanza tangu mwaka 1961.
“Hapana shaka kwamba historia ya hivi karibuni ya Italia ni onyo, nafikiri jambo kubwa tulilofanya baada ya Euro 2020 ni mechi yetu ya kwanza ugenini dhidi ya Hungary, na tulicheza katika kiwango bora, nafikiri ni hivyo,” alisema Southgate.
“Fikra zetu tangu mwanzo zilikuwa vizuri mno, sitarajii fikra hizo zigeuke kuwa tatizo lakini ni kama kukumbushwa kwamba hatua za mwanzo za kufuzu ni muhimu sana,” alisema.
“Nakumbuka tulivyofunga bao la dakika za lala salama dhidi ya Poland kwenye Uwanja wa Wembley kukiwa hakuna mashabiki na kuna ambao watauchukulia ushindi huo kuwa ni kitu rahisi lakini lilikuwa ni tukio muhimu katika kufuzu, tulikuwa na matukio mengi ya aina hiyo siku za nyuma katika mechi za kuwania kufuzu,” alisema Southgate.
“Ingawa mwisho wa siku makundi hayo yalionekana kuwa rahisi lakini kuna mechi nyingi ambazo hali ilikuwa tofauti,” aliongeza Southgate ambaye anawania kushinda mechi ya 50 akiwa kocha England.
Mechi za kufuzu Euro 2024 zitakazopigwa leo Alhamisi usiku ni kama ifuatavyo…
Italia v England
Kazakhstan v Slovenia
Bos-Herze v Iceland
Portugal v Liechtenstein
Slovakia v Luxembourg
North Macedonia v Malta
Denmark v Finland
San Marino v Northern Ireland
