Na mwandishi wetu
Baada ya kupanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, timu ya Kitayosce imebadilishwa jina rasmi na kuwa Tabora United.
Tabora United inayotumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora imefanikiwa kupanda Ligi Kuu NBC ikiungana na mabingwa JKT Tanzania ambao wamerejea kwa mara nyingine.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Adam Simba alisema kuwa baada ya kupanda daraja sasa timu hiyo imebadilishwa jina na kuwa Tabora United na jina la Kitayosce limekufa rasmi.
“Kwa hiyo shughuli yetu kubwa na mikakati yetu endapo tutasajili vizuri na morali tuliyonayo hatuendi kushiriki ligi kuu msimu ujao bali tunaenda kupambana na kuonyesha upinzani mkubwa,” alisema Simba.
“Tunataka kusuka kikosi bora ambacho kitakuwa na mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na vijana, lengo letu ni kuurejesha mkoa wa Tabora kwenye ramani ya soka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” alisema Simba.
Ni kama vile Tabora United imefuata nyayo za DTB ambayo baada ya kupanda daraja msimu wa 2021-22 ilibadili jina na kuitwa Singida Big Stars.