Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
Yanga leo Jumamosi imeanza vizuri maandalizi ya msimu mpya wa 2023-24 kwa kuibwaga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini bao 1-0 katika mechi ambayo pia inahitimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, alikuwa ni Kennedy Musonda aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 45 akimalizia pasi nzuri ya nyota mpya wa Yanga, Maxi Nzengeli.
Musonda baada ya kuunasa mpira huo aliambaa nao kidogo naye akaudokoa kwa juu na kumshinda kipa wa Chiefs, Itumeleng Khune ambaye alitoka hatua chache mbele ya lango lake na hatimaye akajikuta akiushuhudia mpira ukijaa wavuni.
Mara tu baada ya kuingia bao hilo, Khune alimkimbilia mshika kibendera na kuanza kumlalamikia wakati wachezaji wa Yanga wakimkimbilia Musonda kwa ajili ya kumpongeza kwa bao hilo.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Yanga waliutawala vyema mchezo wakipata nafasi kadhaa za kufunga lakini walishindwa kuzitumia hasa Musonda ambaye baadaye alirekebisha makosa yake.
Kipindi cha pili kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko ya wachezaji 10 kasoro kipa, Metacha Mnata, mabadiliko hayo yalizidi kuipa uhai Yanga na kuendelea kulisakama lango la Chiefs lakini mashambulizi hayo hayakuzaa matunda.
Kama ilivyokuwa kwa Gamondi, kocha wa Chiefs, Molefi Ntseki naye alifanya mabadiliko ya wachezaji wengi, mabadiliko ambayo licha ya kuonekana pia kuipa uhai timu hiyo kwa kufanya mashambulizi ya hapa na pale lakini haikuweza kupata bao.
Clement Mzize aliyeingia kipindi cha pili alianza kwa kuichachafya Chiefs mapema katika kipindi hicho kabla ya Chiefs nao kujibu mapigo dakika 10 baadaye.
Mzize mfano katika dakika ya 75 aliuwahi mpira wa krosi uliopigwa na Lomalisa na kuunganisha kwa kichwa lakini kipa Khune alikuwa makini na kuzuia hatari hiyo langoni mwake.
Zikiwa zimebaki dakika 19 mpira kumalizika, kipa namba moja wa Yanga msimu uliopita wa 2022-23, Djigui Diarra naye aliingia kuchukua nafasi ya Mnata.
Kwa ujumla mechi hiyo imeonekana kuwa hatua muhimu kwa makocha Gamondi wa Yanga na Ntseki wa Chiefs kujua nini cha kufanya katika msimu mpya wa 2023-24 kwa michuano ya ndani na ile ya klabu barani Afrika kwani imewapa fursa ya kuwajaribu wachezaji wao wengi wakiwamo wale wapya.
Kimataifa Wiki ya Mwananchi yapendeza
Wiki ya Mwananchi yapendeza
Read also