Paris, Ufaransa
Washambuliaji Kylian Mbappe na Erling Haaland wamekuwa na siku nzuri katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizochezwa usiku wa Jumatano.
Mbappe alifunga bao la kwanza dakika ya 32 wakati timu yake ya PSG ikiichakaza AC Milan mabao 3-0 wakati Haaland alifunga mabao mawili Man City ikitoka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Young Boys.
Kwa upande wa PSG mabao mengine ya timu hiyo yalifungwa na Kolo Muani dakika ya 53 na bao la mwisho lilifungwa na Lee Kang-in dakika ya 89 na kuifanya timu hiyo ishike usukani katika Kundi F.
Bao hilo la Mbappe limemuwezesha mshambuliaji huyo kuwa na rekodi ya kuvutia tangu kuanza kwa
msimu huu akiwa amefunga mabao 13 katika mechi 13 za PSG na timu ya taifa ya Ufaransa.
Matokeo hayo yanazidi kuiweka pabaya Milan ambayo inashika mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi mbili tu katika mechi tatu.
Kwa upande wa mabingwa watetezi Man City, waliokuwa ugenini Switzerland, waliutawala vyema mchezo wao na Young Boys wakiandika bao la kwanza dakika ya 48 lililofungwa na Manuel Akanji lakini Young Boys walisawazisha muda mfupi baadaye kwa bao la Meschack Elia.
Baada ya hapo ndipo umahiri wa Haaland ulipojidhihirisha akifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 68 kabla ya kumalizia bao la pili dakika ya 86.
Matokeo hayo yameifanya Man City kujiimarisha katika usukani kwenye Kundi G na kuwa katika mwelekeo mzuri wa kulipigania taji la michuano hiyo ambalo walilibeba msimu uliopita.
Kwa Haaland sasa anakuwa amefunga mabao kwa mara ya kwanza baada ya kucheza mechi sita, rekodi ambayo hapo kabla ilianza kuibua hofu akionekana kama anaanza kunyemelewa na ukame wa mabao.
Matokeo mechi za Ligi ya Mabingwa Jumatano
Barcelona 2-1 Shakhtar Donetsk
Celtic 2-2 Atl Madrid
Newcastle 0-1 B Dortmund
PSG 3-0 AC Milan
Young Boys 1-3 Man City
Feyenoord 3-1 Lazio
RB Leipzig 3-1 Red Star Belgrade
Royal Antwerp 1-4 FC Porto