Paris, Ufaransa
Sasa ni rasmi, kiungo wa Juventus, Paul Pogba hatokuwamo katika kikosi cha timu ya Ufaransa kitakachokwenda Qatar kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa kuwa anahitaji muda zaidi wa kupona maumivu ya goti baada ya kufanyiwa operesheni.
Pogba hakuichezea Juventus msimu huu tangu ajiunge nayo kwa mara nyingine akitokea Manchester United baada ya kuumia goti mwezi Julai na hatimaye akaamua kufanyiwa upasuaji kwa imani kuwa angeweza kupona na kupata nafasi ya kuiwakilisha Ufaransa kutetea Kombe la Dunia.
Awali ilielezwa kwamba Pogba mwenye umri wa miaka 29 alikuwa njia panda kushiriki michuano hiyo lakini sasa imethibitishwa rasmi kwamba uwezekano wa mchezaji huyo kupona na kuiweza kuiwakilisha Ufaransa kwenye Kombe la Dunia haupo. Ufaransa itajitupa uwanjani katika mechi ya kwanza Novemba 22 dhidi ya Australia.
Taarifa ya mchezaji huyo iliyopatikana leo Jumatatu kupitia wakala wake, Rafael Pimenta ilieleza, “Baada ya ukaguzi wa madaktari jana na leo mjini Torino na Pittsburg, tunasikitika kuarifu kuwa Paul Pogba bado atahitaji muda zaidi ili aweze kupona.”
“Kwa sababu hiyo, Paul hatoweza kujiunga na kikosi cha Juventus kabla ya mapumziko ya fainali za Kombe la Dunia na pia hatokuwamo kwenye kikosi cha Ufaransa kitakachokwenda Qatar,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Mara ya mwisho Pogba aliichezea Ufaransa Machi mwaka huu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini, mechi ambayo Ufaransa ilishinda kwa mabao 5-0 lakini mapema mwezi uliopita alikuwa kwenye kambi ya timu hiyo akifanya mazoezi kabla ya kuamua kufanyiwa operesheni ambayo ilimuweka mbali na soka ingawa wiki mbili zilizopita alianza kufanya mazoezi mepesi katika klabu ya Juventus.
Vyombo vya habari nchini Italia viliripoti kuwa mchezaji huyo alipata maumivu ya misuli ambayo yanazidi kumuweka katika wakati mgumu kupona haraka wakati kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri hivi karibuni alisema kwamba ni vigumu Pogba kupona kabla ya fainali za Kombe la Dunia.
Kimataifa Rasmi, Pogba kukosa Kombe la Dunia
Rasmi, Pogba kukosa Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
