Madrid, Hispania
Aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales amefungiwa na Fifa kujihusisha na mambo yote yanayohusu soka kwa miaka mitatu kwa kosa la kumpiga busu mdomoni mchezaji wa timu ya Hispania, Jenni Hermoso.
Rubiales alimpiga busu mchezaji huyo Agosti 20 mara baada ya Hispania kuibwaga England katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) na kubeba taji hilo.
Jenni ambaye ni mshambuliaji wa timu ya Hispania baadaye alisema hakukuwa na makubaliano yoyote kati yake na Rubiales katika jambo hilo.
Busu hilo liligeuka mjadala mkubwa duniani kote hali iliyomfanya Rubiales mwezi Septemba atangaze kujizulu nafasi ya urais kwenye Shirikisho la Soka Hispania licha ya awali kudai kwamba hangekuwa tayari kuchukua uamuzi huo kwa kuwa haoni kosa alilolifanya.
Jumatatu hii Fifa ilitangaza adhabu ya kumfungia Rubiales miaka mitatu kwa kwenda kinyume na ibara ya 13 ya kanuni za nidhamu za Fifa ingawa ametangaza nia ya kukata rufaa.
“Nitakwenda katika hatua ya mwisho ili kuona haki inapatikana na ukweli unadhihirika,” alisema Rubiales kupitia mitandao ya kijamii.
Awali Fifa ilimsimamisha Rubiales kwa siku 90 kujihusisha na soka na kuahidi kulifanyia uchunguzi tukio zima la kumpiga busu mchezaji huyo ambalo pia limelalamikiwa na viongozi wa kiserikali nchini Hispania.
Rubiales pia amefikishwa mahakamani mjini Madrid kwa kosa la udhalilishaji kijinsia na ukatili na iwapo mahakama itamkuta na hatia katika kosa hilo huenda akakumbana na rungu la dola.
Kimataifa Aliyembusu mchezaji ‘jela’ miaka mitatu
Aliyembusu mchezaji ‘jela’ miaka mitatu
Read also