Seoul, Korea Kusini
Nyota ya mshambuliaji Marcus Rashford imeanza kung’ara katika klabu ya Barcelona baada ya kufunga bao lake la kwanza katika ushindi ya mabao 5-0 dhidi ya timu ya Daegu FC ya Korea Kusini.
Kikosi cha Bacelona au Barca kwa sasa kipo Korea Kusini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2025-26 ambao utaanza rasmi kutimua vumbi baadaye mwezi huu.
Ikiwa hii ni mechi yake ya tatu kwa timu hiyo tangu ajiunge nayo mwezi uliopita kwa mkopo akitokea Man United, Rashford alifunga bao hilo katika dakika ya 65 baada ya kuunganishiwa pasi na Eric Garcia.
Kwa ujumla Barca ilitawala mchezo huo uliopigwa Jumatatu hii huku wapinzani wakishindwa kuonesha makali yao, hawakuweza hata kupiga shuti moja lenye malengo kwenye lango la Barca.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Barca, Hansi Flick alisema wamemaliza hatua muhimu ya maandalizi ya msimu mpya na jambo zuri ni kwamba wameweza kufanya mazoezi yao vizuri.
“Tumemaliza hatua muhimu tumekiona kile ambacho tulikuwa tukitaka kukiona na majaribio yalikuwa mazuri kwa upande wetu,” alisema Flick.
Mabao mengine ya Barca yalifungwa na Robert Lewandowski, Toni Fernández na Gavi ambaye alifunga mabao mawili.
Kwa upande mwingine mchezaji nyota wa timu hiyo, Lamine Yamal ingawa hakufunga bao katika mechi hiyo lakini alionekana kuwa mwiba kwenye lango la wapinzani kwa kuongoza mashambulizi ya mara kwa mara.
