Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Harry Kane amepania kujiunga na klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani ambayo inadaiwa kujipanga kuwasilisha ofa ya mchezaji huyo kwa mara ya tatu.
Tayari Bayern imeshawasilisha ofa mbili za kumtaka nahodha huyo wa Engand huku ofa ya pili ikidaiwa kufikia Dola 103 milioni na sasa huenda ofa ya tatu ikaboreshwa zaidi.
Kane ambaye pia anadaiwa kuwindwa na PSG na Real Madrid, atakuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu ujao wa 2023-24, inadaiwa pia amepania kuhakikisha anajiunga na wababe hao wa Ujerumani.
Habari za ndani zinadai kwamba kocha wa Bayern, Thomas Tuchel alikutana na mchezaji huyo jijini London wiki chache zilizopita na Kane mwenyewe alivutiwa na mpango huo akiamini ataenda kubeba mataji na timu hiyo.
Inadaiwa kwamba kaka wa mchezaji huyo ambaye pia ndiye wakala wake, katika siku za karibuni amekuwa na mazungumzo na mabosi wa Bayern yaliyojadili uhamisho wa mchezaji huyo.
Wakati Bayern ikiendelea na harakati hizo, kocha mpya wa Spurs, Ange Postecoglou alisema kwamba hawezi kuwa na uhakika wa kuwa na mchezaji huyo ingawa angependa kufanya naye mazungumzo mara baada ya mchezaji huyo kumaliza mapumziko na angependa abaki katika timu hiyo.
Habari nyingine zinadai kwamba pamoja na Bayern kumtaka Kane lakini klabu hiyo iko makini katika ofa itakayotolewa huku mabosi Spurs wakipania kuvuna pesa ndefu kupitia mshambuliaji huyo mwenye rekodi za kuvutia za mabao.
Kimataifa Kane apania kwenda Bayern
Kane apania kwenda Bayern
Read also