Na mwandishi wetu
Droo ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake imepangwa leo huku timu ya Simba Queens ikipangwa Kundi A dhidi ya timu za Asfar Club ya Morocco, Green Buffaloes (Zambia) na Determine Girls (Liberia).
Simba ambao ni wawakilishi pekee kutoka Afrika Mashariki walikata tiketi ya michuano hiyo baada ya kuibuka mabingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kuifunga She Corporates ya Uganda kwa bao 1-0 kwenye fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wiki mbili ilizopita.
Timu nyingine zilizounda Kundi B la michuano hiyo ambayo droo yake ilifanyika jijini Rabat, Morocco ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Bayelsa Queens (Nigeria) na Wadi Degla (Misri). Aidha, Kundi B linasubiri bingwa wa Ukanda wa Umoja wa Shirikisho la Afrika ya Kati ili kukamilisha idadi ya timu nne za kundi hilo.
Michuano hiyo inatarajia kuanza kuunguruma Oktoba 30 mpaka Novemba 13, mwaka huu nchini Morocco baada ya mchujo wa kila kanda ulioanza kufanyika tangu Agosti 7, mwaka huu.
Michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya pili tangu ilipoanzishwa msimu uliopita, bingwa wake mtetezi ni Mamelodi waliotwaa taji hilo kwa mara ya kwanza wakiifumua Hasaacas Ladies ya Ghana kwa mabao 2-0 katika fainali iliyopigwa Cairo, Misri.
Soka Simba Queens Kundi A Ligi ya Mabingwa
Simba Queens Kundi A Ligi ya Mabingwa
Read also
