Na mwandishi wetu
Mabao mawili ya Maxi Nzengeli yameiwezesha Yanga kutoka na ushindi wa 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Singida Big Stars iliyopigwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo wa Yanga uliopatikana kwa mabao ya kipindi cha kwanza umeifanya timu hiyo kutulia kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 18 katika mechi saba ilizocheza hadi sasa.
Maxi aliandika bao la kwanza kwa Yanga katika dakika ya 30 ya mchezo huo akiujaza mpira wavuni kwa kichwa baada ya kuinasa krosi iliyochongwa na beki wake Yao Kouasi.
Dakika saba kabla ya mwamuzi kupulizi filimbi ya kumaliza kipindi cha kwanza, Nzengeli aliandika bao la pili safari hii akifunga kwa shuti kali akiwa nje kidogo ya eneo la 18.
Singida ilijikuta ikipata pigo baada ya kuumia kwa kipa wake, Benedict Haule ambaye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Kashindi.
Katika harakati za kutaka kusawazisha mabao waliyofungwa, Singida iliwatoa Habib Kyombo na Duke Habuya na nafasi zao kuchukuliwa na Deus Kaseke na Frank Kazadi ambao hata hivyo hawakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Kwa upande wa Yanga wao walimtoa Mudathir Yahya na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Abubakar au Sure Boy na baadaye kuwatoa Hafiz Konkoni na Pacome Zouazoua na kuwaingiza Kennedy Musonda na Skudu Makudubela.
Singida nao waliamua kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji kwa kumuingiza Meddy Kagere akichukua nafasi ya Aziz Andambwile lakini Kagere au MK47 naye alishindwa kuitungua ngome ya Yanga.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa Ijumaa hii, Azam FC ikiwa nyumbani Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ilijikuta katika wakati mgumu baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 mbele ya Namungo FC.
Matokeo hayo yanaibua hali ya wasiwasi kwa Azam ambao msimu huu wamekuwa wakijinadi kuwa na dhamira ya kulibeba taji la ligi lakini matokeo hayo yanakuwa sawa na kuiweka njia panda dhamira hiyo.
Nazo Tanzania Prisons na KMC zikiwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam zilitoshana nguvu kwa kutoka uwanjani na sare ya bao 1-1.