Na mwandishi wetu
Mshambuliaji nyota wa Yanga, Fiston Mayele amesema anatamani mno kubeba tuzo ya mfungaji bora katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Kwa sasa mshambuliaji huyo ndiye kinara wa mabao akiwa amefunga mabao matano sawa na mshambuliaji hatari wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivavilo.
Akizungumza leo Jumatano mshambuliaji huyo amesema ili kuhakikisha ndoto zake zinatimia amewaomba wachezaji wenzake kumpa ushirikiano kwa kumchezesha ili aweze kufunga.
“Malengo ya timu yanabaki kwenye ubingwa na ubingwa unakuja kutokana na kufunga mabao kwa sababu mimi ni miongoni mwa wachezaji waandamizi kwenye kikosi cha Yanga ndio maana nimewaomba wenzangu wanisaidie kunichezesha ili nitimize malengo ya timu na yangu,” alisema Mayele.
Mshambuliaji huyo ameeleza kuwa kwake itakuwa na maana kubwa katika soka kama atafanikiwa kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo makubwa ya Caf na anaamini hilo linawezekana kutokana na ushirikiano mzuri alionao na wachezaji wenzake.
Alisema mbali na hilo, Yanga kwa sasa ina kikosi bora na ndio maana wamefika hatua hiyo na anaamini kama wataongeza juhudi wana uwezo wa kufika fainali na kubeba taji hilo.
Mbali na Kombe la Shirikisho lakini Mayele pia anaongoza kwa ufungaji kwenye Ligi Kuu NBC akiwa amefunga mabao 16 mpaka na anapewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo ya mfungaji bora msimu huu.
Msimu uliopita, Mayele alishindwa kuibeba tuzo hiyo ambayo ilichukuliwa na George Mpole aliyekuwa akikipiga Geita Gold.