Paris, Ufaransa
Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi ameamua kumtolea uvivu mshambuliaji, Kylian Mbappe akimtaka aamue kama anataka kubaki katika klabu hiyo lazima asaini mkataba mpya vinginevyo hawako tayari kumuacha aondoke mwakani akiwa mchezaji huru.
Mbappe aliiweka PSG mtegoni mapema mwezi uliopita baada ya kuandika barua akiuarifu uongozi wa klabu hiyo hana nia ya kuongeza mkataba wake wa sasa unaofikia ukomo mwaka 2024.
Baadaye Mbapppe alifafanua kwamba hakuwahi kuuomba uongozi wa klabu hiyo umruhusu ahamie Real Madrid, klabu ambayo siku za nyuma ilijaribu kumshawishi ajiunge nayo lakini ilishindikana.
PSG imejikuta ikiwa njia panda kuhusu hatma ya Mbappe kama imuache amalizie mwaka mmoja katika mkataba wake na imuache aondoke akiwa huru na kuifanya timu hiyo ishindwe kupata chochote kwa mchezaji iliyemnunua mwaka 2017 kwa ada ya Dola 195.7 milioni kutoka AS Monaco.
“Msimamo wangu upo wazi, sitaki kurudia kila wakati kama Kylian anataka kubaki, sisi tunamtaka abaki lakini anahitaji kusaini mkataba mpya,” alisema Al-Khelaifi wakati wa kumtangaza kocha mpya wa timu hiyo Luis Enrique.
“Hatutaki kumpoteza mchezaji bora duniani aondoke akiwa mchezaji huru, hatuwezi kufanya hivyo, hii ni klabu ya Ufaransa,” alisema Mbappe.
“Amesema hawezi kuondoka akiwa huru, kama leo amebadili mawazo hilo si kosa langu, hatutaki kumuacha mchezaji bora duniani aondoke akiwa mchezaji huru, hilo lipo wazi,” alisema.
Mbappe amemaliza msimu uliopita wa 2022-23 na PSG akiwa mfungaji bora na amefanya hivyo kwa misimu minne iliyopita, PSG inapenda kuendelea kuwa na mchezaji huyo hasa baada ya kuondoka kwa Lionel Messi.