Porto, Ureno
Kocha wa timu ya Ureno, Roberto Martinez amesema hakuna wa kutilia shaka habari kuwa Cristiano Ronaldo anaweza kucheza katika fainali za Kombe la Dunia 2030 wakati huo akiwa na miaka 45.
Ronaldo atakuwa na timu ya Ureno kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazotarajia kutimua vumbi Juni 11 katika nchi za Marekani, Mexico na Canada, hii ikiwa ni mara ya sita kwa mchezaji huyo kushiriki fainali hizo.
Fainali za Kombe la Dunia 2030 zitafanyika kwa ushirikiano katika mataifa ya Mexico na Hispania na Martinez anaamini kwa wakati huo haitokuwa ajabu jina la Ronaldo kuwamo kwenye kikosi cha Ureno.
Ronaldo alianza kuichezea Ureno mara ya kwanza mwaka 2003, kwa sasa ndiye anayeongoza kuichezea timu hiyo mara nyingi (226) akiwa amefunga mabao 143 na ni mchezaji pekee mwenye rekodi ya kufunga mabao katika fainali tano za Kombe la Dunia.
Martinez aliulizwa swali iwapo Ronaldo ataweza kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2030 ambapo kocha huyo alisema hakuna anayeweza kutilia shaka jambo hilo.
Kauli ya Martinez imekuja wakati Ronaldo mwenyewe hajaweka wazi ni lini hasa atastaafu kuichezea timu hiyo hivyo haitokuwa ajabu akiwa na timu hiyo.
Ronaldo ambaye pia amewahi kutamba na timu za Man United na Real Madrid, kwa sasa anacheza soka Saudi Arabia katika klabu ya Al Nassr akiwa ndiye mchezaji anayelipwa fedha nyingi.
Ureno ipo Kundi K, itacheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia Juni 17 dhidi ya DR Congo na kufuatiwa na mechi dhidi ya Uzbekistan Juni 23 na kumalizia mechi za makundi dhidi ya Colombia Juni 27.
Kimataifa Ronaldo atajwa Kombe la Dunia 2030
Ronaldo atajwa Kombe la Dunia 2030
Read also
