Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Yanga imetozwa faini ya Sh milioni 30 kwa kosa la wachezaji wake na maofisa wa benchi la ufundi kukataa kutumia chumba kilichotengwa kwa ajili ya kubadilishia nguo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamhuyo, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea wakati wa mechi baina yao na Simba iliyochezwa Mei 3, 2026 kwenye uwanja huo ambapo Yanga inadaiwa badala yake walitumia nyumba iliyo karibu na uwanja huo kitendo ambacho ni kinyume na kanuni.
Adhabu hiyo imetokana na kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kilichokaa Mei 9, 2026 na taarifa hiyo kutolewa Jumatatu Mei 10, 2026 na tayari klabu hiyo imeanza kuembeza bakuli ikiomba kuchangiwa fedha hizo na wanachama na mashabiki wake.
Katika adhabu hiyo, meneja wa Yanga Walter Harson pia amefungiwa mechi tatu pamoja na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kumsukuma kiungo wa Simba, Clatous Chama.
Yanga pia imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani siku ya mechi hiyo, ambapo badala ya kuwasili saa 10:30 alasiri wao waliwasili saa 10:35 yaani dakika tano baadaye.
Katika adhabu hizo hizo, shabiki wa Yanga aliyetajwa kwa jina la Mohamed Mposo ambaye amekuwa akiambatana na maofisa wa ufundi wa klabu hiyo amefungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi 12.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shabiki huyo anadaiwa kuingia kwenye eneo la kuchezea wakati wa mapumziko jambo ambalo ni kinyume cha sheria lakini pia alionekana akimwaga vimiminika tukio ambalo linahusishwa na ushirikina.
Nayo klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh milioni tano kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya kabla ya mechi yao na Mtibwa Sugar na kufika wakiwa pungufu bila ya vifaa vyote vinavyohitajika kwa mujibu wa taratibu.
Katika Ligi ya Championship, klabu ya Hausung FC ya Njombe imetozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kuchelewa kwa dakika 20 kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi yao na Geita Gold.
Mchezaji Said Kubwa wa TMA FC amefungiwa michezo mitatu na faini ya Sh 500,000 kwa makosa yanayohusishwa na vitendo vya ushirikina kwa kumwaga vimiminika uwanjani, katika mechi yao na Gunners FC.
Adhabu kama hiyo pia imetolewa kwa Mohamed Lipangala na Joel Stephano pia wa TMA ambao pia wanadaiwa kuonekana wakichimba vitu kwenye nguzo za goli la timu yao, vitendo vyote hivyo vinahusishwa na ushirikina.
Klabu ya Hausung imepoteza mchezo wake na Mbeya Kwanza kwa kosa la kushindwa kufika uwanjani bila sababu, badala yake Mbeya Kwanza imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Hausung pia kwa kosa hilo hilo imetozwa faini ya Sh milioni moja pamoja na mwenyekiti wake, Erasto Haule kufungiwa kujihusisha na soka kwa kipindi cha miezi 12.
Kimataifa Yanga yapigwa faini Sh milioni 30, yatembeza bakuli
Yanga yapigwa faini Sh milioni 30, yatembeza bakuli
Read also
