Paris, Ufaransa
Kocha Mauricio Pochettino hatimaye anatarajia kuondoka katika klabu ya PSG huku kukiwa na utata kuhusu kocha na mchezaji wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane kumrithi.
Katika siku za hivi karibuni, Zidane au Zizou ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na timu hiyo, mpango ambao ulikolezwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Rais Macron alinukuliwa wiki iliyopita akisema kwamba angekuwa tayari kumshawishi Zizou kuwa kocha nchini Ufaransa japo alisema kwamba hajazungumza lolote na kocha huyo aliyeweka rekodi Real Madrid kwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa mchezaji na baadaye kocha.
Pochettino raia wa Argentina inadaiwa amekutana na mabosi wa PSG kujadili hali ilivyokuwa msimu wa 2021/22, msimu ambao aliiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1 lakini alikwama katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutolewa na Real Madrid katika hatua ya 16 bora. Madrid ndio waliotwaa taji hilo baada ya kuifunga Liverpool bao 1-0 katika mechi ya fainali.
Kwa kuwa mkataba wa Pochettino na PSG unafikia ukomo mwaka 2023 ni wazi kwamba kuna mambo ya kufanyiwa kazi, kubwa likiwa ni maslahi yake pamoja na mambo mengine kabla ya kuondoka kwake Ufaransa ikiwa ni siku chache baada ya mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo naye kufutwa kazi na nafasi yake kukabidhiwa, Luis Campos.
Wakati ikiaminika kuwa Zizou ndiye atakayemrithi Pochettino, zipo habari kwamba kocha huyo hayuko tayari kujiunga na PSG jambo ambalo linawaweka katika wakati mgumu matajiri wa klabu hiyo kuanza kumfikiria kocha mwingine wa hadhi kama ya Zizou atakayeipa mafanikio timu hiyo hasa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mbali na Zizou ambaye hajaonyesha utayari wa kuitaka PSG, kocha mwingine anayetajwa kurithi mikoba ya Pochettino ni Christophe Galtier wa Nice.
