Ligi Kuu yasimamisha usajili Ihefu
Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila ameeleza kuwa kwa sasa hawana haraka ya kufanya usajili kwa ajili ya msimu ujao kutokana na kuendelea kwa mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Championship.
Katwila amefafanua kuwa mara kadhaa ukifuata wachezaji kwenye kipindi cha mechi za mwisho wa ligi huwa hawana maamuzi sahihi kutokana na changamoto ya mechi hizo za mwishoni hivyo ni bora watulie kwanza mpaka ligi zitakapomalizika kabisa.
“Kutokana na kusubiri kumalizika kwa mechi za Ligi Kuu na zile za ‘play-off’ za Champioship, tutautumia muda huu sasa kuandaa ripoti ambayo tutawapa viongozi kisha waturejeshee na sisi tuione halafu tutajua usajili wetu unaanzia wapi.
“Kikosi chetu tutakuwa na baadhi ya mabadiliko kuelekea Ligi Kuu msimu ujao tukifahamu pia ugumu wa ligi unabadilika kulingana na msimu wenyewe na wakati mwingine hautabiriki, kwa hiyo sisi tunajipanga kwa ajili ya changamoto hizo mpya, tunaamini tutapambana nazo,” alisema Katwila.
Ihefu ndiyo mabingwa wa Championship msimu huu ikiwa imemaliza kinara kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 66 sawa na DTB iliyomaliza nafasi ya pili isipokuwa wanatofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
