Na mwandishi wetu
Ikiwa ni siku tatu tu zimepita tangu timu ya Singida Big Stars imtambulishe kipa Metacha Mnata, leo imetangaza kusajili kipa mwingine Benedict Haule kutoka Tanzania Prisons alikokuwa kwa mkopo akitokea Azam FC.
Imeelezwa kuwa Haule aliyewahi kuidakia Mbao ya Mwanza kabla ya kutua Azam amepewa kandarasi ya mwaka mmoja katika timu yake hiyo mpya.
Ujio wa Haule katika kikosi hicho umeibua hisia za pengine Singida wameanza kuziba pengo la Metacha mapema ambaye usajili wake unatajwa kuwa una utata baada ya timu aliyotoka ya Polisi Tanzania kubainisha kuwa bado wana mkataba wa mwaka mmoja na kipa huyo.
Hata hivyo, GreenSports imezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Singida, Muhibu Kanu kufahamu zaidi kuhusu usajili huo ambapo amefafanua kuwa makipa wote hao wapo kwenye mipango yao na ishu ya Metacha itapatiwa ufumbuzi hivi punde.
“Tumeingia mkataba na Haule ni miongoni mwa wachezaji tuliokuwa tukiwapigia hesabu, usajili wake hauhusiani chochote na Metacha. Ishu ya Metacha tumewasikia Polisi walichokisema na tumewaambia waje tuzungumze nao hapo kwenye utata na tupate ufumbuzi.
“Sisi tumejiridhisha na vitu vingi ikiwemo mchezaji mwenyewe, baadhi ya watu anaoshirikiana nao na tumejiridhisha kwa baadhi ya mambo muhimu kuwa tunamsajili kihalali lakini kama kuna tatizo tupo tayari kuzungumza na Polisi,” alisema Kanu.
Mbali na Metacha, hivi karibuni timu hiyo pia iliingia kwenye utata wa usajili wa mshambuliaji Habib Kyombo ambaye pia ilielezwa amemalizana na Simba lakini baadaye viongozi wa timu hizo walikaa mezani na Kyombo akatambulishwa upya Simba kama mchezaji wao halali.
Soka Benedict Haule asajili Singida Stars
Benedict Haule asajili Singida Stars
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
