Berlin, Ujerumani
Mwanasoka na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Franz Beckenbauer amefariki dunia akiwa na miaka 78 akiacha rekodi ya kubeba Kombe la Dunia akiwa mchezaji mwaka 1974 na baadaye kocha mwaka 1990.
Beckenbauer (pichani) ambaye alikuwa beki, mbali na timu ya taifa pia alitamba na Bayern Munich, timu ambayo aliichezea mechi 582 wakati kwenye timu ya taifa amecheza jumla ya mechi 103.
Mbali na mataji ya dunia, Beckenbauer ambaye alipewa jina la utani la ‘Der Kaiser’, pia wakati akiichezea Bayern alibeba taji la Ulaya mwaka 1972 na kushinda tuzo ya Ballon d’Or mara mbili.
Taarifa ya familia ya mchezaji huyo iliyopatikana Jumatatu usiku ilieleza kusikitishwa na msiba huo wa mume na baba wa familia.
“Kwa masikitikio makubwa tunatangaza kuwa mume wangu na baba yetu, Franz Beckenbauer amefariki kwa amani akiwa usingizini usiku wa Jumapili, tunawaomba mtupe nafasi ya kuombeleza kwa ukimya na kujiepusha na kutuuliza maswali yoyote,’ ilieleza taarifa ya familia hiyo.
Taarifa ya klabu ya Bayern ambayo aliichezea kwa mafanikio ilimpamba Beckenbauer kwa kumtaja kuwa ni mmoja wa wanasoka muhimu na mwenye mafanikio.
“Dunia ya Bayern Munich ghafla imekuwa tofauti na ilivyozoeleka, kumekuwa na kiza, ukimya na unyonge, Bayern isingeweza kuwa ilivyo sasa bila ya Beckenbauer,” ilieleza taarifa hiyo.
Beckenbauer enzi zake za soka la ushindani alikuwa akicheza nafasi ya kiungo na anakumbukwa zaidi kwa namna alivyokabana na Sir Bobby Charlton katika mechi ya fainali za Kombe la Dunia 1966, mechi ambayo England ilishinda kwa mabao 4-2 ingawa baadaye Bckenbauer alihamia nafasi ya beki.
Katika fainali za Kombe la Dunia 1966, Beckenbauer alifunga mabao manne na alishinda tuzo ya mchezaji mwenye umri mdogo aliyeshiriki fainali hizo, wakati huo alikuwa na miaka 20.
Beckenbauer ni kati ya wachezaji watatu duniani wenye rekodi ya kubeba Kombe la Dunia wakiwa wachezaji na baadaye makocha.
Katika orodha hiyo yumo Mario Zagallo wa Brazil ambaye alifariki majuzi akiwa na miaka 92 na Didier Deschamps wa Ufaransa ambaye kwa sasa ndiye mchezaji na kocha pekee mwenye rekodi hiyo aliye hai.
Kimataifa Beckenbauer afariki dunia
Beckenbauer afariki dunia
Read also