Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kwamba timu yake imeporwa ushindi katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns baada ya kutolewa kwa penalti 3-2.
Yanga usiku wa kuamkia Jumamosi hii ilitolewa lakini timu hiyo ilipata bao dakika ya 59 mfungaji akiwa Aziz Ki ambaye shuti lake liligonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani ingawa picha zilionesha mpira huo ulivuka mstari wa goli.
Kukataliwa kwa bao hilo kuliifanya mechi imalizike kwa dakika 90 matokeo yakiwa sare ya 0-0 kabla ya kuingia kwenye mikwaju ya penalti na Yanga kulala kwa penalti 3-2.
Akiizungumzia mechi hiyo, Gamondi alisema ilikuwa nzuri na kuisifu timu yake kwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ingawa baada ya hapo hakutaka kuzungumzia mechi hiyo kwa kile alichodai kwamba kila kitu kilionekana.
Akifafanua kuhusu bao la Aziz Ki, kocha huyo alihoji ni kwa nini mwamuzi wa mchezo huo hakuwa tayari kwenda kuangalia VAR kujiridhisha badala yake alitegemea kupewa taarifa ingawa alifanya hivyo katika rafu ya Lomalisa, alijiridhisha na kumpa kadi ya njano.
Kocha huyo alikataa maswali na kusema kwamba Wananchi milioni 30 wa Tanzania wameporwa ushindi na kusisitiza kwamba kama kuna nia ya kulinda heshima ya soka la Afrika ni vyema kuanzia na tukio hilo.
“Shinda mechi ni sawa, hakuna tatizo lakini shinda kwa haki, heshima ya Watanzania leo imeporwa kwa kweli lile lilikuwa goli la wazi au kuna mtu anataka kujadiliana na mimi kuhusu hilo akiamini si goli, aseme,” alisema Gamondi kwa Kiingereza ambacho hakikuwa kizuri.
“Kama watu wa Sundowns wanafurahia hilo ni sawa lakini soka haliko hivyo, tunazungumzia Fair Play, Fifa wanazungumzia Fair Play,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alifafanua kuwa hiyo ni mara ya pili anaporwa ushindi, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2018 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika alikutana na tukio kama hilo la kuporwa ushindi.
Alisema kwamba mwamuzi anaweza kufanya makosa kwa kuwa yeye ni binadamu lakini kwa nini hakwenda kuangalia VAR kujiridhisha badala yake alisema anajiamini lakini alimshangaa kwa kitendo cha kumpa kadi mchezaji wake (Lomalisa) baada ya kujiridhisha.
Gamondi alisema timu yake imepambana na timu bora ya Afrika na imefuzu Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza lakini inaishia kuporwa ushindi kwa namna ile.