Na mwandishi wetu
Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said amesema wako kwenye majadiliano na mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa kuhusiana na sakata lao la udhamini mpya wa Kampuni ya Haier.
Hersi amesema pamoja ya kuwa kwenye mgongano na SportPesa kwa sasa lakini iko wazi kuwa kampuni hiyo ndiyo wadhamini wao wakuu na kwamba wameingia mkataba na Haier kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika pekee.
Alisema hata hivyo, mchakato wote huo wa kumpata mdhamini mpya waliwashirikisha SportPesa kwa kila hatua ingawa hawezi kuweka hadharani kila kitu kwa sasa mpaka watakapomaliza mazungumzo waliyonayo sasa.
“Haier ni mdhamini wa Yanga kwenye mashindano ya Caf (Shirikisho la Soka Afrika) ambayo SportPesa hawezi kuwepo kutokana na taratibu za kikanuni za mashindano juu ya kuwa na mdhamini anayefanya michezo ya kubahatisha.
“Kupitia muktadha huo tuliona sababu za kutafuta mdhamini anayeweza kukaa hapo lakini kwa mashauriano na SportPesa, tumefanya mawasiliano na yote tunayo katika kila hatua na pia hata baada ya kumpata mdhamini huyu, hivyo vyote siwezi kuviweka hadharani sababu ni mawasiliano rasmi baina yetu na SportPesa,” alisema Hersi.
Hersi aliongeza kuwa bado wanaendelea kujadiliana, kueleweshana kwamba maamuzi waliyoyachukua wanafikia kwenye makubaliano mazuri na SportPesa na baada ya kukamilika taratibu za kiutendaji ambazo ziko ndani ya ofisi, wataueleza umma walichoafikiana na kinachoendelea.
“Niweke sawa kwamba tuna uhusiano mzuri sana na SportPesa, ndiyo mdhamini wetu mkuu, hata Jumamosi tukicheza na Namungo tutavaa jezi zetu za udhamini wa SportPesa na nisingependa kueleza kila kitu sasa.
“Tutakapokuwa tumekamilisha vitu vyote tutakuja hadharani kueleza kila kitu baada ya sakata hili sasa kuanza upya kutokana na barua ya SportPesa kwa umma na kwetu pia kutaka maelezo zaidi ya hii kitu,” alisema Hersi.
Hayo yameibuka baada ya SportPesa juzi kueleza kutoridhishwa na maamuzi ya Yanga kuitangaza Haier kama mdhamini mpya kwenye michuano ya Caf licha ya kuwapa maelezo kuwa watumie nembo ya Visit Tanzania badala ya kutafuta mdhamini mpya na sasa inaomba msaada kwa mamlaka husika kwa uharibifu uliosababishwa.
Mwanzoni mwa msimu huu, Yanga ilihuisha mkataba wake na SportPesa kwa kusaini dili la miaka mitatu lenye thamani ya Sh bilioni 12.3 kabla ya Januari 30, mwaka huu kutangaza kuingia mkataba na Haier wa Sh bilioni 1.5 mahsusi kwenye michuano ya Caf pekee.
