Eldoret, Kenya
Mwanariadha wa Uganda aliyeiwakilisha nchi hiyo kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, Rebecca Cheptegei amefariki dunia siku chache baada ya kuchomwa moto na rafiki yake wa kiume.
Rebecca, 33, aliungua zaidi ya asilimia 70 ya mwili wake baada ya kuchomwa moto na rafiki yake wa kiume baada ya kuibuka mzozo baina ya wawili hao.
Msemaji wa Hospitali ya Moi ya mjini Eldoret, Owen Menach alithibitisha kuwa mwanariadha huyo amefariki leo Alhamisi asubuhi baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo siku chache zilizopita akiwa na hali mbaya na viungo vyake vingi kushindwa kufanya kazi.
Rebecca alishiriki vyema Michezo ya Olimpiki ya Paris akiwa mwakilishi wa Uganda na kumaliza nafasi ya 44 katika mbio za marathon kwa wanawake na umauti umemkuta akiwa hajamaliza hata mwezi mmoja tangu kuiwakilisha Uganda kwenye Olimpiki.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya hospitali hiyo, Joseph Cheptegei ambaye ni baba mzazi wa Rebecca alisema amepoteza mtoto ambaye alikuwa msaada mkubwa kwake na ana matumaini haki itatendeka.
Mapema Jumatatu taarifa ya polisi wa kaunti ya Trans-Nzoia, ilieleza kuwa rafiki wa kiume wa Rebecca alitumia galoni la petroli na kummwagia Rebecca kabla ya kumuwashia moto.
Moto huo hata hivyo uliwaunguza wote wawili na hadi sasa rafiki huyo naye amelazwa katika hospitali hiyo hiyo akiwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu.
Awali kiongozi wa eneo lililotokea tukio hilo alisema wawili hao walikuwa na mzozo ambao chanzo chake kinadaiwa ni eneo la ardhi ambalo lina nyumba inayodaiwa kujengwa na Rebecca, nyumba ambayo tukio la moto huo lilitokea.
Shirikisho la Riadha Uganda lilitoa taarifa kupitia mitandao ya kijamii kueleza kusikitishwa na kifo cha Rebecca na kumuombea marehemu apumzike kwa maani huku wakilaani tukio zima la mauaji hayo na kuomba haki itendeke.
Mwanariadha aliyechomwa moto afariki dunia
Read also
