London, England
Nyota wa zamani wa Man United, Louis Saha ameamua kumtolea uvivu Cristiano Ronaldo kwa kumwita mbinafsi anayejiangalia yeye zaidi.
Saha ambaye amewahi kucheza katika klabu ya Man United na Ronaldo na kuna wakati alidaiwa kuvutiwa na mafanikio ya mchezaji huyo hadi kuiga utaratibu wake wa mazoezi, amedai kwamba Ronaldo anazungumzia mambo yasiyo na uhalisia kwa kutaka kwake kuvunja mkataba na klabu hiyo.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 sasa, ameshaweka wazi nia yake ya kutaka kuondoka katika klabu hiyo lakini kinachoonekana ni kwamba wakala wake Jorge Mendes licha ya kufanya juhudi kumtafutia timu ya hadhi yake, inaonekana kumekuwa na ugumu kuipata timu hiyo hali inayomfanya abaki kuwa mchezaji wa Man United jambo ambalo Ronaldo anaona ugumu kulikubali.
Mazingira hayo ndiyo yaliyomuibua Saha ambaye anamuona mchezaji huyo mwenzake wa zamani kuwa ni mbinafsi ingawa alitahadharisha kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na hitimisho la moja kwa moja kwa mambo anayofanya Ronaldo.
Saha alisema: “Mimi si Cristiano lakini ni mtu ambaye naweza kuwa katika nafasi ya mashabiki wa Manchester United, naona ni kama vile haonyeshi kwamba sasa inatosha kwa kile anachokifanya, anajifikiria yeye mwenyewe.”
“Siwezi kumfanyia tathmini na kuwa na hitimisho la moja kwa moja kwa sababu ni mchezaji muhimu na mimi sipo katika nafasi yake lakini ningependa kuona anabaki Man United kwa sababu ni mchezaji mkubwa, kwa sababu ni mchezaji mzuri na hakuna wa kumfanyia tathmini kwa sababu tu ya kile anachotaka kwenye maisha yake binafsi ya soka,” alisema.
Shauku ya Ronaldo kutaka kuihama Man United kwa kiasi kikubwa inadaiwa kuchangiwa na timu hiyo kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo anataka Man United ivunje mkataba wake na kumruhusu aondoke akiwa mchezaji huru kwani hataki kucheza Europa Ligi, michuano ambayo hakuwahi kuicheza na pengine anaona si hadhi yake.
Katika hilo Saha anasema Ronaldo anataka mambo yasiyo na uhalisia kwa kudhani kuwa Man United wanaweza kuvunja mkataba wake na kumpa ruhusa ya kuondoka kwa sababu tu msimu uliopita mambo hayakuwa mazuri.
Ronaldo hakushiriki katika ziara ya maandalizi ya msimu wa 2022/23 ya timu hiyo katika nchi za Thailand na Australia kwa kile kilichodaiwa kuwa ni matatizo ya kifamilia lakini habari zisizo rasmi zilidai kuwa alichofanya ni mgomo baridi kushinikiza kuruhusiwa aondoke katika klabu hiyo.
Jumapili iliyopita kwenye dimba la Old Trafford, Ronaldo alifanya kitendo kilichoshangaza wengi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Rayo Vallecano ambayo ilikuwa mechi yake ya kwanza kwenye timu hiyo tangu kumalizika kwa msimu wa 2021/22.
Baada ya kucheza kwa dakika 45 za kwanza na kutolewa, Ronaldo baadaye alionekana akitoka nje ya uwanja wakati mechi ikiendelea, maofisa wa Man United walikataa kusema lolote kama aliruhusiwa na kocha Erik ten Hag au aliamua tu kujiondokea huku timu hiyo ikitoka sare ya bao 1-1 huku bao la Man United likifungwa na Amad Diallo aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Ronaldo.
Klabu za Bayern Munich, Barcelona na Atletico Madrid zimewahi kuhusishwa na mchezaji huyo lakini zote baadaye kwa nyakati tofauti zilijiweka kando na mpango huo, pia amewahi kutakiwa na klabu kdhaa za Marekani na moja ya Saudi Arabia kwa mikataba inayotajwa kuwa minono lakini Ronaldo mwenyewe hajashawishika kujiunga na timu hizo.
Kimataifa Saha: Ronaldo mbinafsi
Saha: Ronaldo mbinafsi
Read also